Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, anatarajiwa kuongoza Mkutano wa Mawaziri wanaohusika na masuala ya Fedha na Uwekezaji wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jopo la Mapitio ya Uchumi Mpana (Peer Review Panel) unaotarajiwa kufanyika tarehe 15 Julai 2020 kwa njia ya mtandao kutokea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es salaam.
Mkutano huu utatanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara za Fedha na Benki Kuu wa SADC, utakaofanyika kwa siku mbili kuanzia kesho tarehe 13-14 Julai, 2020.
Mkutano huu ambao utawakutanisha Mawaziri wenye dhamana na masuala ya Fedha na Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi 16 wanachama wa SADC, utajadili masuala ya Fedha na Uwekezaji pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji katika mkutano uliofanyika mwezi Julai 2019, Windhoek, Namibia.
Vilevile mkutano huu utajadili kwa kina na kutoa maamuzi ya kisera kuhusu athari za Kiuchumi na Kijamii za COVID-19.
Mkutano huu ulipangwa kufanyika ana kwa ana kuanzia tarehe 13-17 Julai, 2020 lakini kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19), utafanyika kwa njia ya mtandao kuanzia tarehe 13 hadi 15 Julai, 2020 .
Mkutano huu ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkutano wa dharura wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika tarehe 18 Machi 2020, Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, ulimuelekeza Mwenyekiti wa Baraza kwa kushirikiana na Sekretarieti ya SADC kusimamia zuio la kufanyika kwa mikutano ya ana kwa ana kutokana na mlipuko wa COVID-19.
Imetolewa na
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
Social Plugin