MWALIMU ATIWA MBARONI JIJINI MBEYA KWA WIZI WA MILIONI 34


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia JOSEPH SHILA [29] Mwalimu Shule ya Msingi Mwakareli na Mkazi wa Mwakareli kwa tuhuma za wizi wa fedha Tshs.Milioni 34,000,000/= mali ya mwalimu mstaafu GIDEON NGOLAKO MWALUJOBO [60] Mkazi wa Mwakareli.

Kwa Mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei , Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 30.06.2020 majira ya saa 19:00 Usiku huko Kijiji na Kata ya Mwakareli, Tarafa ya Busokelo, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya baada ya kupata taarifa toka kwa msiri. 

Amesema mtuhumiwa alifanikiwa kuiba pesa hizo mali ya mwalimu mstaafu GIDEON NGOLAKO MWALUJOBO [60] Mkazi wa Mwakareli kupitia akaunti 6140201871 kwa kutumia “NMB Mobile” katika Tawi la NMB Mbalizi Road baada ya kupata namba ya siri ya mhanga ambaye walikuwa ni Walimu wa Shule moja na marafiki wa siku nyingi.

Amesema mtuhumiwa pia anajihusisha na uwakala wa kusajili laini za simu kwa kutumia mfumo wa kisasa wa alama za vidole ambapo aliweza kutengeneza laini ya simu kwa jina la Mhanga na kutokana na kuaminiana na mhanga pia alikuwa ana mpa kadi yake ya Benki kwa ajili ya kumtolea fedha.

Katika upekuzi uliofanywa nyumbani kwa mtuhumiwa amekutwa na fedha taslimu Tshs.Milioni 20,780,000/=, Kadi ya Benki NMB, Simu tatu [03] aina ya Tecno na laini mbili za simu. 

Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ulrich Matei ametoa wito kwa wananchi kuwa makini na kadi zao za benki ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatunza namba ya siri ili kujiepusha na matukio ya wizi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post