Na Said Mwishehe, Michuzi TV.
VIONGOZI wa kada mbalimbali nchini wameendelea kuelezesha kusikitishwa kwao na taarifa za kifo cha Rais Mstaafu katika Serikali ya Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa ambacho kimetokea usiku wa kumkia leo Julai 24, 2020 jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, kila kiongozi amemuelezea mzee Mkapa kwa jinsi alivyomfahamu ambapo kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk.Harson Mwakyembe amesema si rahisi sana kupata msamiati sahihi kueleze hisia alizonazo kutokana na kifo cha mzee Mkapa ambaye ndiye alimuibua alipokuwa kijana mdogo anafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipokuwa akifundisha kitivo cha Sheria.
"Aliniteua kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uandishi wa Habari wakati huo kilichokuwa kinaitwa TSJ.Ni mzee Mkapa ayeniteua kuwa moja ya wakurugenzi wa kwanza wa Benki ya NBC baada ya kubinafsishwa , ni Rais Mkapa ndiye aliyeniingiza kwenye masuala ya utumishi wa umma, kwa kweli kifo chake kinaacha ombwe kubwa moyoni mwangu kama vile mtu anavyoondokewa na mzazi wake,"amesema Dk.Mwakyembe.
Alipoulizwa ni lini amepata nafasi ya kuzungumza na Mzee Mkapa, Dk.Mwakyembe amesema alikuwa akipata fursa ya kukutana naye mara kwa mara lakini sio kwa mazungumzo marefu lakini amepata bahati ya kukaa karibu naye, hivyo ataenzi yale yote mazuri yaliyofanywa na Mkapa na atayaendeleza.
Kwa upande wake mwanasiasa mkongwe nchini Profesa Juma Kapuya ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Magharibi mwaka 1995 amesema amepokea taarifa za kifo hicho kwa masikitiko makubwa sana na kwamba kama ni hazina basi nchi imepoteza hazina kubwa.
"Kwa kweli ni pigo kwa nchi kwasababu , pengo lake halizibiki, na ukweli kabisa kama ni hazina basi nchi imepoteza hazina kubwa. Katika watu waliokuwa wanasimamia kwa kauli thabiti umoja wa Taifa hili, ni mzee Mkapa ambaye alikuwa anasimamia kwa dhati kabisa umoja wa kitaifa.Pia maono yake kwa maendeleo ya nchi, tunakumbuka wakati anachukua nchi mwaka 1995 hali ilivyokuwa alivyojitahidi kurudisha heshima ya nchi hii ilikuwa ni miujuza.
"Mimi nilikuwa kwenye baraza lake la mawaziri, nikiwa na mzee Lowasa, tulikuwa tunafanya kazi usiku na mchana.Ndani ya miezi tisa ya utawala wake akarudisha heshima na hata wafadhili nao wakaanza kurudi, walianza kuitambua Tanzania kama nchi yenye dira ambayo inaeleweka katika maaendeleo.Pia nakumbuka mzee Mkapa alikuwa hamrishi, unajenga hoja na kisha mnajadiliana kwa hoja mpaka mnafika mahala mnakubaliana,"amesema Profesa Kapuya.
Alitoa mfano ulipojitokeza mjadala huko nyuma kuhusu kufutwa kwa adhabu ya viboko na lugha ya Kingereza ambapo mjadala ulikuwa mkubwa sana." Walikuwa wanataka shule zote zifundishe Kiswahili na fimbo zifutwe shuleni, akaniita Waziri mbona haya yanazungumzwa sana lakini sijakusikia ukitoa kauli? Nikambambia sawa mzee , lakini nikamjibu fimbo mimi sifuti kwasababu utamadani wa kufuta fimbo shuleni hatujaufikia, Ulaya mimi nimeishi sana , darasa kubwa sana lina watoto 12.Lakini shule zetu wakati huo darasa moja watoto zaidi ya 200 katika darasa moja,mwalimu anapata wapi nafasi ya kuzungumza na mtoto mmoja mmoja.
"Kwa hiyo mzee utamaduni haujafikia pale, halafu tukaja kwenye Kingereza, nikamwambia hao wanaotaka tufundishe kwa Kiswahili wanakudanganya , watoto wao hawasomi hapa, hao ni wanafiki lakini pia kisiasa mbele ya safari itatuletea matatizo , kwasababu kazi mbele ya safari kazi itakuwa inachukua waliosoma na wanaojua lugha mbalimbali.
"Hivyo watoto wengi ambao hawajui Kingereza hawatapata kazi, hivyo haiwezekani kwani hii nchi ni yetu wote.Hivyo tulikubaliana na baadae nikatangaza,"amesema Profesa Kapuya na kuongeza kuwa mzee Mkapa alikuwa ni rafiki yake na katika ujenzi wa Uwanja wa Taifa watu wote wanakumbuka lakini kifo chake ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
Wakati huo huo Waziri Mkuu mstaasfu Joseph Warioba amesema yeye alimfahamu kwa mara ya kwanza mzee Mkapa mwaka 1964 na tangu wakati huo wakawa wanaelewana na baadae wakakutana kwenye utumishi wa umma.
"Nakumbuka hata wakati tunaingia kwenye baraza la mwisho la mawaziri la Nyerere vijana ambao tulipata nafasi nilikuwa mimi, Mkapa, Makweta na Salim.Ni vijana ambao tulikuwa na muelekeo unaofanana , hivyo tangu wakati huo tukawa tunafanya kazi kwa karibu sana.Hata nilipokuwa Waziri Mkuu yeye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje, ni wakati ambao tuliendelea kufanya kazi kwa karibu sana.
"Baada ya kuja mfumo wa vyama vingi mwaka 1995 ikawa sasa tupate Rais mpya , Mkapa akawa ananiambia mimi nigombee na mimi namwambia yeye agombee, hivyo tukaingia kwenye kinyang'anyiro kila mmoja akiwa na mtandao wake , tukaenda mikoani kupata wadhamini, mtandao wake na mtandao wangu ukawa unafanya kazi kwa pamoja , mmoja akitangulia mahali kupata wadhamini basi anawaandaa wadhamini kwamba mwenzangu anakuja.
"Na hata tulipokwenda Lindi, tulikwenda pamoja na tukakutana na wazee.Hata baada ya kuchaguliwa na kuingia kwenye hatua ya tatu mimi sikuchaguliwa, hivyo mtandao wangu ukaungana na mtandao wake. Wakati wote tulikuwa karibu sana na hata alipoingia madarakani tuliendelea kushirikiana na nilikuwa mshauri wake kwenye mambo mengi,"amesema Warioba.
Hata hivyo amesema Rais mstaafu Mkapa ni moja kati ya watanzania waliokuwa wa kweli katika uzalendo , alikuwa mtu muadilifu sana kwa nchi yake na alikuwa anapenda kusoma na kujifunza zaidi ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha."Kifo chake ni pigo kubwa sana katika nchi yetu,"amesema Warioba wakati akimuelezea Mkapa na jinsi walivyokutana na kufanya kazi pamoja.
Social Plugin