NAIBU WAZIRI MHE.KANYASU AZUNGUMZA NA WANUNUZI WAKUBWA WA MALIGHAFI KUTOKA SHAMBA LA MITI SAO HILL


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amekutana na kufanya mazungumzo  Wanunuzi Wakubwa wenye viwanda  wanaonunua  malighafi inayozalishwa kutoka katika Shamba la Miti Sao Hill lililopo katika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Akizungumza  jana mkoani Iringa  kwa nyakati tofauti na Uongozi wa Wamiliki wa Viwanda hivyo, Mhe.Kanyasu amesema   lengo la ziara hiyo ni kutaka kujua changamoto wanazokabiliana   nazo wakati wanapohitaji malighafi hizo  ili kuweza  kuzitafutia  ufumbuzi na kujua  jinsi gani mlipuko wa virusi vya Corona ulivyoathiri katika Uzalishaji wao.

Katika ziara hiyo, Mhe.Kanyasu alitembelea Kiwanda cha Kuzalisha Karatasi cha Mgololo ( MPM) na  Kiwanda cha Kuzalish nguzo za Umeme (Mufindi Woodpoles and Timber LTD)

" Nimeamua kufanya ziara hii ili kuweza kukutana na Wawekezaji ambao ni wateja wakubwa  wa shamba hili,  Kama Wizara tumeona ni muhimu wa kuwatembelea ili kuweza  kuwasikiliza na endapo kama wana changamoto ziweze kushughulikiwa haraka" alisisitiza Mhe.Kanyasu.

Akizungumza na Wanunuzi hao kwa nyakati tofauti, Wanunuzi hao wamemueleza kuwa wamekuwa wakipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Meneja wa Shamba la Miti Sao Hill pindi wanapohitaji Malighafi kwa ajili ya Viwanda vyao bila vikwazo vyovyote.

" Mimi kama Waziri mwenye dhamana nimefarijika sana kusikia kutoka kwa Wanunuzi hawa kuwa wamekuwa hawapati changamoto yoyote wakati wanapohitaji Malighafi kutoka  Shamba la Miti Sao Hill" alisema Kanyasu

Aidha,  Mhe.Kanyasu amesema ziara hiyo imekuwa muhimu kwa sababu imetoa nafasi kwa Serikali kujitathmini na pia imewapa nafasi Wateja wa Shamba hilo kusema hisia zao kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya Muuzaji na Wanunuzi wa Malighafi za mazao ya Misitu.

Katika hatua nyingine Mhe.Kanyasu amesema ugonjwa wa Corona  umewaathiri kwa kiasi Wazalishaji hao licha ya kuwa  waliendelea na uzalishaji kama kawaida lakini bidhaa zao hazikuweza kusafirishwa kwenda nchi za nje kutokana na baadhi ya nchi kufunga mipaka yao.

Kwa upande wake Mhandisi Mkuu Msaidizi wa Kiwanda cha Kuzalisha Karatasi cha Mgololo, Gregory Chogo amemshukuru Naibu Waziri huyo kwa kuonesha kuwathamini na kuwajali wateja wa Shamba hilo kwa kuamua kuwatembelea baadala ya kusubiri  kuletewa taarifa mezani.

Amemuhakikishia kuwa wataendelea kununua malighafi katika Shamba hilo kadri ya mahitaji kufuatia ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka kwa Uongozi wa Shamba hilo na endapo kutakuwa na vikwazo hawasita kusema ili vitatuliwe.

Hata hivyo, Mhandisi Chogo amemueleza kuwa kwa sasa Kiwanda kimesimama uzalishaji kutokana na janga la Corona kwa sababu bidhaa zilizolishwa tayari hazijaanza kusafirishwa nchi za nje.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post