Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ameagiza wasimamizi wa uchaguzi ndani ya chama hicho kuhesabu kura zote mbele ya wajumbe wa mikutano.
Akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma Rais Magufuli amesema kama ilivyofanyika kwenye vikao vya kutafuta wagombea wa Urais, kura zihesabiwe mbele ya wajumbe ili kila mmoja ajue kwa uwazi amepata nini.
Mchakato wa kura za maoni kwa chama hicho unafanyika kwa siku mbili leo na kesho Jumanne.
Rais Magufuli amesema wanachama 10,367 wa CCM wametia nia kugombea ubunge na uwakilishi nchi nzima ambapo waliokamilisha taratibu na kuzirejesha ni 10,321.
“Nilikua napata taarifa leo kwa ajili ya kugombe nafasi mbalimbali katika nchi nzima, walikuwa ni 10,367 na katika hao wamekamilisha taratibu na kurudisha fomu ni 10,321, kwa hiyo hawakurudisha 46 katika nchi nzima,” amesema Rais Magufuli.
Mwenyekiti huyo wa CCM amewataka wasimamizi wa kura za maoni, waendeshe michakato hiyo kwa uwazi bila mizengwe, ili mtia nia anayestahili kupendekezwa kugombea katika uchaguzi huo, apate haki yake.
Rais Magufuli amesema zoezi la kuhesabu kura lifanyike kwa uwazi mbele ya wajumbe, kama ilivyofanyika katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), wa kutuea mgombea Urais wa Tanzania na Zanzibar.