Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI ATOKWA MACHOZI AKIMWELEZEA HAYATI RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifuta machozi wakati akielezea namna alivyomjua Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa wakati akihutubia katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
***
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, amejikuta akitokwa machozi hadharani baada ya shindwa kujizuia wakati akielezea mazungumzo yake ya mwisho na Rais mstaafu awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa.

Hilo limejitokeza leo Jumanne tarehe 28 Julai 2020 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kulipokuwa kunafanyika shughuli ya kuaga Kitaifa mwili wa Mkapa aliyefariki dunia Alhamisi tarehe 23 Julai 2020 saa 3:30 usiku kwa mshituko wa moyo.

Akihutubia taifa katika shughuli hiyo iliyohudhuriwa na maelfu ya waombolezaji uwanjani hapo, Rais Magufuli amesema hakuna mtu anayeweza kumwelezea vizuri Mzee Mkapa zaidi alivyojieleza mwenyewe vizuri kwenye kitabu chake cha My Life, My Purpose.(Maisha Yangu, Kusudio Langu).

Katika hotuba yake, Rais Magufuli ambaye alikuwa mara kadhaa anatulia, akilengwa lengwa na machozi amesema kifo cha Mkapa ni pigo kubwa kwa taifa.


“Binafsi niliongea na Mzee Mkapa kwa simu saa chache kabla hajafariki, nakumbuka aliniambia “John usiwe na wasiwasi naendelea vizuri”.  Sikujua yale maneno yalikuwa ya kuniaga, namshukuru Mungu kwa zawadi ya Mzee Mkapa ya kuwa naye pamoja.

“Mzee Mkapa alikuwa na sifa ya kulea vipaji vya uongozi na kuvikuza, yeye ndiye aliniibua mimi lakini kama mtakavyokumbuka alimchagua mzee Kikwete kuwa Waziri wa Mambo ya Nje miaka kumi ambaye baadaye alikuja kurithi kiti chake cha urais.

“Mzee Mkapa ni shujaa wangu, hata nilipopatwa na shida Mzee Mkapa hakuniacha kamwe, hakutaka nianguke, alinilea kama mtoto wake, saa nyingine machozi yanakuja lakini hata Kikwete nilimuona siku ile analia kwa hiyo msinishangaeshangae.

“Watanzania wanamkumbuka Mzee Mkapa kwa mageuzi ya uchumi, wakati anaingia madarakani nchi yetu ilikuwa na matatizo ya kiuchumi, na wakati huo alianza kulipa madeni na kuanza kuzishawishi taasisi za kifedha pamoja na nchi wahisani kufuta madeni yake.

“Mzee Mkapa amefariki dunia ikiwa imepita miezi nane tu tangu azindue kitabu chake cha My life, My purpose tarehe 12 Novemba 2019, ambapo ndani ya kitabu hicho ameeleza kwa kirefu sana historia ya maisha yake.” amesema  Magufuli.

CHANZO - MWANAHALISIONLINE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com