Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amelegeza kwa kiasi fulani sheria kali zilizokuwa zimewekwa kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Akilihutubia taifa hilo leo Jumatatu katika Jumba la Harambee jijini Nairobi, Rais Kenyatta ametangaza kuondoa marufuku ya safari ya watu kuingia au kutoka katika kaunti za Nairobi, Mombasa na Mandera kuanzia kesho Jumanne.
Hata hivyo amesema kuwa agizo la kutotoka nje kuanzia saa tatu usiku hadi saa kumi alfajiri litaendelea kuwepo kwa kipindi cha siku 30 zijazo.
Vile vile, Rais Uhuru Kenyatta amesema makanisa na misikiti itafunguliwa lakini waumini wasiozidi 100 ndio watakaoruhusiwa kuhudhuria ibada na kwa muda usiozidi saa moja. Shule za Jumapili na madrasa zitasalia kufungwa kwa muda wa siku 30.
Hali kadhalika Rais wa Kenya amesema safari za ndege za ndani ya nchini zitaanza Julai 15, huku zile za kimataifa zikitazamiwa kuanza Agosti Mosi, lakini kwa kufuata tahadhari za kiafya.