Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa akionesha mashuka kitenge kimoja, ndala zinazodaiwa kuwa za Asha Mwandu Makwaiya Mkazi wa Majengo Mapya Mjini Shinyanga alizotaka kuzigawa kwa wajumbe wa Jumuiya ya Wanawake CCM (UWT).
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Wakati joto la uchaguzi likiendelea kushika kasi,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga linamshikilia Mjumbe wa CCM Mkutano Mkuu Taifa CCM, Asha Mwandu Makwaiya Mkazi wa Majengo Mapya Mjini Shinyanga kwa kosa la kutoa rushwa kwa wajumbe wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT).
Kwa Mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya habari ilitolewa na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa leo Jumatano Julai 1,2020 Asha Mwandu Makwaiya alikamatwa Juni 28,2020.
“TAKUKURU katika ufuatiliaji wa vitendo vya Rushwa kuelekeza kipindi hiki cha uchaguzi ilimkamata Bi. Asha Mwandu Makwaiya ambaye ni mkazi wa Majengo Mapya Shinyanga Mjini na Mjumbe wa CCM Mkutano Mkuu Taifa akiwa nyumbani kwa Elizabeth Donald Itete ‘Mama Buzwizwi’ ambaye ni Katibu wa UWT tawi la Mshikamano pamoja na wajumbe wengine 10 ambao ni viongozi wa UWT kata ya Ngokolo”,amesema Mussa.
“Bi. Aisha Mwandu Makwaiya alitaka kugawa mashuka 10, kitenge kimoja, ndala 11 kwa wajumbe 11 wa umoja wa Jumuiya ya Wanawake CCM (UWT) kata ya Ngokolo kama kishawishi cha yeye kuchaguliwa au kuchaguliwa kwa aliyemtuma”,ameongeza Mussa.
Aidha amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU kama ambavyo wamekuwa wakifanya ili kuhakikisha kuwa kero ya rushwa katika mkoa wa Shinyanga inaondolewa mkoani Shinyanga hasa katika kipindi hiki cha michakato ya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Social Plugin