Msanii wa muziki wa Bongo fleva na Mjasirimali hapa nchini Zuwena Mohamed maarufu kama ‘Shilole’, amevunja ukimya na kukiri kuwa huwa anapewa kichapo sana na mumewe Ahrafu Sadiki maarufu ‘Uchebe’ jambo ambalo ameshindwa kulivumilia.
Akizungumzia hilo kupitia kwenye Ukurasa wake wa Instagram Shilole ameandika walaka mzito juu ya shutuma hizo, kuhusu mumewe anavyompiga na kumuumiza vibaya na kusema kwa sasa ndoa imemshinda.
“Naandika haya, nikiwa na akili timamu na utulivu, la kwanza kabisa Naomba radhi kwa jamii yangu, kwa sababu niliwaaminisha ndoa yangu haina tatizo, huku ukweli ukiwa hauko hivyo, nimekuwa mtu wa kuambulia vipigo na mengine yasiyozungumzika, Naomba radhi kwa sababu niliposikia wanawake wenzangu wakipigwa niliwaambia Pazeni suti, niliposikia mwanamke kule Kigamboni ameuwawa na kuchomwa moto niliomboleza na jamii na kusema Bora angesema, huku mimi nikijikausha na kujitoa kwenye kundi lao wakati ukweli wangu Mimi ni mwenzao, Naomba radhi.
“Mimi ni kioo cha jamii, tena sura kubwa ya wanawake. Leo nimeona nivunje ukimya kwa kuweka wazi kwamba Mume wangu Ashrafu Sadiki maarufu kama ‘Uchebe’, ananipiga sana, na tena hata baada ya kunipiga hajali kupiga simu wala kujua naendeleaje, nauguzwa na watu baki hospitali, na bado manyanyaso mengine yanayoikosesha hii ninayoiita Ndoa uhai na furaha.
“Na zaidi nina watoto wanaoniangalia kama Baba na Mama, leo nikubali kufa na kuacha wanangu barabarani, sitweza. Uchebe ni mwanaume niliyempenda, nilimvumilia kwa madhaifu yote, nikampa kila kitu, (Utu wangu, Mali Zangu na hata palipotakiwa kumuendeleza asimame mwenyewe nilifanya kwakuwa nilijua tuko pamoja), lakini hilo halikuwahi kuzuia vipigo, dharau na usaliti.
“Siku mbili zilizopita baada ya kutoka Sabasaba kutafuti watoto wangu na kumtafutia yeye nilipigwa sana, sababu za kupigwa ni migogoro midogo ya kawaida ambayo ipo kwenye kila ndoa, sio kwamba amenifumania au mambo yanayoshindwa kuzungumzika, hapana, tena namuheshimu sana, lakini solution aliyoiona ni kunipiga kinyama bila huruma, tena kwa kunishtua na ngumi nikiwa usingizini, Kama mnavyoona picha hapo ni matukio ya siku tofauti tofauti.
“Najua nitalaumiwa kwa kuweka hili mtandaoni, ila sina namna, maisha yangu ni maisha ya watu kwa kiasi kikubwa, jamii inanitazama kama mfano. Nimefika mwisho, na kuanzia sasa naomba nisitambulike kama Mke wa Uchebe, ila Mama alieamua kuweka maslahi ya watoto wake mbele na kuamua kuwa mwenyewe kwa usalama na furaha yake
“Wakati nahangaikia mambo yangu ya ndoa, post hii itumike kuwakumbusha wanawake Tuvunje ukimya, tupinge ukatili, tutakuja kuuliwa bila sababu,” ameandika Shilole.
Social Plugin