Aliyekuwa Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Shinyanga Azza Hamad akijinadi kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wilaya ya Shinyanga kuomba kura za kuchaguliwa kuwa mgombea wa jimbo la Solwa.
Na Damian Masyenene – Shinyanga Press Club Blog
MCHAKATO wa watia nia wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya ya Shinyanga Vijijini kwa ajili ya kupiga kura za maoni kumchagua mgombea wa chama hicho atakayepeperusha bendera kwenye jimbo la Solwa mkoani Shinyanga unaendelea katika Uwanja wa Kambarage mjini humo kwa watia nia 54 kujieleza.
Ambapo mchakato wa watia nia kujieleza umeanza saa 8 mchana, ambapo aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Ahmed Salum ndiye aliyekuwa wa kwanza kujieleza, huku akiahidi kulifanya Jimbo la Solwa kuwa kama nchi ya Japan.
Ahmed ambaye amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa muda wa miaka 15 (2005-2020) amesema jimbo hilo lilikuwa zero (sifuri) na sasa linang’aa kila mtu analitamani kupitia miradi mingi iliyotekelezwa kwenye sekta ya umeme, maji na afya, huku mingine ikiwa njiani kuanza utekelezaji.
“Nimefanya kazi ambayo nyie wenyewe mnaijua na wagombea wengi wanalitamani, nimetamani kugombea tena ili Kukamilisha kazi ndogo iliyobaki na nataka Solwa iwe kama Japan, mpaka kufikia 2025 vijiji vyote viwe na maji ya Ziwa Viktoria,” amesema.
Naye aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azzah Hilal (CCM) ambaye alikuwa mtia nia wa sita kujinadi, amesema baada ya kazi kubwa ya kuutumikia mkoa wa Shinyanga sasa ni muda muafaka wa kulitumikia Jimbo la Solwa.
“Mkinipa ridhaa nitafanyia mambo makubwa, nimefanya mengi kila mtu ni shahidi, nawaomba mnipe mimi kama mama niweze kulilea jimbo la Solwa,” amesema.
Baadhi ya watia nia wengine akiwemo Anitha Lugeye ambaye ameahidi kukomesha rushwa iliyokithiri jimboni humo, pia Amos Maige Kamondo amesema vipaumbele vyake ni Elimu, Afya, vituo vya afya, uwekezaji, sana na michezo.
“Nimejipanga kushughulika na maabara na hosteli katika shule za sekondari, kuongeza gari za dharura za wagonjwa na kuboresha miundombinu,” amesema Kamondo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela amewaomba wapiga kura hao kuwa makini na kuwataka watia nia kuwa na nia njema ya kukitangaza na kukipa ushindi chama hicho, huku akiwaasa kumuunga mkono atakayeteuliwa na kuvunja makundi.
“Ambao kura hazitatosha muendelee kumuunga mkono aliyepita na tujumuike pamoja kukipa ushindi chama chetu, mgombea ambaye atafanya mambo ambayo siyo hatateuliwa hata kama atakuwa Mshindi wa kura za maoni, kwahiyo hatutaki kampeni za kupakana matope na kuhusisha ukabila,” amesema.
Naye Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Vijijini, Ernestina Richard, amewatahadharisha wapambe wa wagombea kuacha shamra shamra kwani bado kuna mchujo mkali, huku akiwataka wanachama kuacha makundi na chuki kwani siyo lazima wote wawe wabunge.
Mchakato huo wa kura za maoni unasimamiwa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya wilaya hiyo, Peter Gawiza, ambapo jumla ya watia nia 54 wa jimbo hilo wanajinadi mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, ambao umehudhuriwa na wajumbe 843 kutoka kata 27 za wilaya hiyo.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM wilaya ya Shinyanga wakisubiri kupiga kura kuchagua atakaye peperusha bendera ya Chama hicho jimbo la Solwa.
Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Solwa Ahmed Salum akiomba kura kwa wapiga kura ili wamchague tena kuwa mbunge wao.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Shinyanga Edward Ngelela akizungumza kwenye Mkutano mkuu wa uchaguzi.
Wajumbe wa Mkutano mkuu
Mgombea ubunge jimbo la Solwa Amos Maige akiomba kura kwa wapiga kura ili aweze kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo,huku akiahidi kufanya mabadiliko makubwa
Mgombea ubunge jimbo la Solwa Amos Mshandete akijinadi kwa wajumbe ili waweze kumchagua kuwa mwakilishi wao.
Wagombea ubunge jimbo la Solwa 54 wakiwa wamekaa wakisubiri kuanza kujieleza na kuomba kura kwa wajumbe,ili aweze kupatikana mgombea mmoja.