Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Musabila Kusaya kusaya amesema Tanzania ina nafasi yakubwa ya kuleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Kilimo ikiwa kila Mdau kwenye mnyororo wa thamani atatimiza wajibu wake ipasavyo.
Katibu Mkuu Kusaya ameyasema hayo, jana tarehe 02/07/2020 wakati wa kikao maalum alichokiitisha ili kujadiliana na Wadau wa zao la chai pamoja na Wazalishaji wa mbolea maalum ya zao la chai; Inayoitwa Minjingu Chai katika Ukumbi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) Jengo la Kilimo I, Jijini, Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Kusaya amesema Mkulima anategemea maendeleo ya utafiti kwenye tasnia ya mbolea, anategemea ushauri mzuri wa Maafisa Ugani, anategemea kwa sehemu kubwa uzalishaji wa mbolea ambao utamuakikishia kupatikana kwa wakati na kwa bei nafuu lakini pia Mkulima anategemea Ushirika imara ili awe na uhakika wa kuuza mazao yake baada ya kuvuna.
Bwana Gerald Kusaya ameongeza kuwa pembejeo moja ya muhimu katika ukuaji wa Sekta ya Kilimo ni mbolea na kwamba mazingira ya Tanzania yanatoa fursa nyingi kwa viwanda vingi kuanzishwa licha ya kukiri kuwa kuna changamoto kadhaa ambazo Serikali imekuwa ikiendelea kuzitatua ili siku moja mazingira ya uwekezaji yawe mazuri kwa kiwangi kikubwa.
Bwana Gerald Kusaya ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuweka jitihada na kuweka mazingira mazuri na wezeshi katika uwekezaji na ujenzi wa viwanda vya mbolea nchini. Aidha, sambamba na jitihada hizo, pia kuna fursa mbalimbali zinazohamasisha uwekezaji katika shughuli za uzalishaji wa mbolea nchini.
Amezitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na: - Uwepo wa utashi wa kisiasa unaoruhusu uwekezaji katika tasnia ya mbolea.
“Tanzania ni kitovu cha usambazaji katika mataifa ya Jumuia ya Afica ‘SADC’ ambayo hayana bandari. Uwepo wa Wahandisi wa Kemikali “Chemical Engineers” wenye taaluma ya kuzalisha mbolea wa kutosha katika soko la ajira.” Amekaririwa Katibu Mkuu Kusaya.
Bwana Gerald Kusaya ametaja fursa nyingine ni pamoja na uwepo wa Vituo vya Utafiti wa mazao ya kilimo; Yanayotumia mbolea. Uwepo na nia ya makampuni binafsi yanayojihusisha na uwekezaji wa mbolea na visaidizi vyake. Kufunguliwa kwa mipaka ya kuuza mazao nje ya nchi inayohamasisha kuwepo kwa mahitaji makubwa ya mbolea na visaidizi vyake.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa kuwepo kwa soko kubwa la ndani na nje la mahitaji ya mbolea na visaidizi vyake. Uwepo wa Miundombinu kama nishati na barabara inayowezesha usafirishaji wa mbolea kutoka bandarini hadi kwa mkulima wa mwisho.
Uwepo wa malighafi za kuendeshea viwanda zinazotokana na mazao ya kilimo ambayo yanazalishwa kwa kutumia mbolea pamoja na uwepo wa viwanda vingi vinavyotumia malighafi za mazao ya kilimo; hivyo kufanya mahitaji ya mbolea kuongezeka.
Aidha Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya amekiri kuwa tasnia ya mbolea inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo; Gharama kubwa za uwekezaji na uzalishaji zinazofanya mbolea zinazozalishwa nchini kuwa na bei kubwa kuliko zinazoingia nchini.
Ameongeza kuwa kuwepo na mifumo ya kisheria yenye utata ambayo inamlazimisha mwekezaji kushughulikia masuala mengine ambayo yanaweza kufanywa na taasisi zingine.
Pamoja na kukosekana kwa ushirikiano “collaboration” na watengenezaji wa bidhaa saidizi kama kutengeneza vifungashio, kuweka maandishi kwenye mifuko.
“Changamoto tajwa hapo juu zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kuundwa kwa jopo la kiwizara ili kuimarisha mahusiano na Ofisi ya Rais TAMISEMI na kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Mbolea Namba 9 ya Mwaka 2009 kuhusu usimamizi wa uwekezaji katika viwanda vya mbolea (Interministerial Commitee).” Amekaririwa Bwana Gerald Kusaya.
Katibu Mkuu Kusaya amesema Bodi ya TFRA inajukumu la kuboresha mazingira ya uwekezaji katika viwanda na kurekebisha sheria ya mbolea na miongozo inayohamasisha Wawekezaji waliopo kuzalisha kulingana na uwezo wa kiwanda.
“TFRA iendelee kusimamia na kuhakikisha kwamba viwanda vyote vya mbolea na visaidizi vyake nchini vinasajiliwa na kuwa na leseni hai muda wote.”
“TFRA iendelea kufuatilia na kutoa ushauri kwa wawekezaji wa viwanda vya mbolea kukamilisha nyaraka zote muhimu zinazotakiwa ili waweze kukidhi vigezo vya kuanzisha viwanda vya mbolea.”
“TFRA iendelee kushirikiana na Taasisi za utafiti na wadau wengine wa maendeleo katika kuelimisha umma juu ya umuhimu wa matumizi sahihi y mbolea.”
“TFRA iendelee kuhamasisha wadau mbalimbali wa kilimo kupitia vyombo vya habari na maonesho ya kilimo ili wawekeze katika tasnia ya mbolea.” Amekaririwa Katibu Mkuu akitoa maagizo hayo kwa Menejimenti na Watumishi wa Mamlaka ya Mbolea nchini (TFRA).
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya yupo Jijini Dar es Salaam, ambapo tangu siku ya Jumanne tarehe 30 Juni, 2020 hadi Ijumaa tarehe 03 Julai, 2020 atakuwa akizitembela Taasisi za Wizara ya Kilimo, zilizopo Jijini, Dar es Salaama na baadae anataraji kuanza ziara ya kutembelea ili kujionea changamoto na maendeleo ya Sekta ya Kilimo mazao katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ziara ambayo inataraji kuanza tarehe 08 Julai, 2020.