Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), tunasikitishwa na kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Uwepo wa vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za wanawake na watoto kama inavyoainishwa katika Ibara ya 12 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inayotaka haki ya kuheshimu na kuthamini Utu wa Mtu.
Licha ya kuwa vitendo hivi ni aibu kwa Taifa kwa ujumla, lakini pia vinakosesha Amani na kusababisha madhara kimwili, kisaikolojia na kiuchumi kwa wahusika na jamii.
TGNP tunakemea vitendo hivyo na kutoa rai kwa mamlaka husika za serikali hususan jeshi la polisi kufuatilia na kuchukua hatua stahiki kisheria.
Vile vile, tunawataka viongozi wa dini kusimama katika nafasi zao na kukemea vitendo hivi; Jamii kutokaa kimya pale ambapo matukio kama haya yanapojitokeza kwa kutoa taarifa kwa mamlaka na vyombo husika.
Pia, tunawataka watu binafsi kujitokeza na kupaza sauti pale wanapoona viashiria au vitendo ya ukatili vikifanyika ndani ya familia na jamii kwa ujumla.
TGNP itaendelea kufuatilia na kupaza sauti dhidi ya matendo haya ya kikatili yanayodhalilisha, na kuondoa Utu na Heshima kwa wanawake na watoto.
TGNP