TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA (THBUB) YATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KIFO CHA RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA


TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) tumepokea kwa majonzi makubwa taarifa ya kifo cha ghafla cha mpendwa wetu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa, kilichotokea usiku wa kuamkia leo Julai 24, 2020 huko jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mfupi.


Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora tunaungana na familia na Watanzania wote katika kuomboleza kifo hiki cha ghafla cha mpendwa wetu Hayati Benjamin William Mkapa.

Tunatoa pole kwa wafiwa wote – wanafamilia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania Wote. Mungu awatie nguvu,  awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Tume inatambua kuwa kifo hiki cha ghafla kimeliondolea Taifa letu nguzo na hazina muhimu ya hekima, busara na maarifa katika uongozi wa nchi, na hususan usuluhishi na utatuzi wa migogoro na changamoto mbalimbali za kitaifa. Lakini tunatambua kuwa lililo muhimu kwa sasa ni kumwombea marehemu wetu pumziko jema.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora tunamkumbuka Hayati Benjamin William Mkapa kwa jinsi alivyothamini na kusimamia misingi ya utawala bora na haki za binadamu hapa nchini wakati wa kipindi chake cha “Zama za Ukweli na Uwazi”.

Hakika hatutazisahau jitihada zake za kupambana na rushwa nchini, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Tume ya Warioba iliyofanya utafiti wa kina kuhusu rushwa hapa nchini, kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kuhimiza uwajibikaji katika kazi.

Aidha, atakumbukwa kwa kuimarisha uchumi na huduma za jamii, kwa kuanzisha Mkakati wa Kuondoa Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania (MKUKUTA); Mpango wa Kurasimisha Mali na Biashara (MKURABITA); Mpango wa Kusaidia Kaya Masikini (TASAF); na Taasisi ya Benjamin Mkapa, ambayo inasaidia sana kuimarisha haki ya huduma ya afya vijijini.

Sambamba na hayo yote Hayati Benjamin William Mkapa atakumbukwa kwa kutunza amani na umoja wa Watanzania na kusuluhisha migogoro barani Afrika.

Tunawaomba Watanzania kuendelea kudumisha amani na umoja wetu hususan katika kipindi hiki cha msiba huu mzito na tunapoelekea katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Mwezi Oktoba mwaka huu; kwa kufanya hivyo tutakuwa tunamuenzi vema mpendwa wetu, Hayati Benjamin William Mkapa.

Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Mpendwa wetu, Hayati Benjamin William Mkapa mahali pema peponi, Amina.

Imetolewa na:
Mhe. (Jaji Mstaafu) Mathew Pauwa Mhina Mwaimu
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Julai 24, 2020


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post