Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : GREYSON KAKURU ACHAGULIWA KUWA MWENYEKITI MPYA WA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA SHINYANGA


Mwenyekiti mpya wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Greyson Kakuru aliyechaguliwa katika mkutano mkuu wa uchaguzi leo Julai 4, 2020.


Na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club Blog
Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club - SPC) leo Julai 4, 2020 imefanya mkutano wake mkuu wa uchaguzi kutimiza matakwa ya kikatiba, ambapo imepata safu mpya ya uongozi.

Katika uchuguzi huo uliosimamiwa na aliyekuwa Diwani wa Kata ya Ndembezi (CCM) Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila umefanyika katika ukumbi wa Mkuu wa mkoa, mjini Shinyanga.

Nafasi zilizokuwa zinagombaniwa ni Wajumbe watano wa kamati tendaji, Mweka hazina, Katibu Msaidizi, Katibu Mtendaji, Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti wa klabu hiyo.

Uongozi uliomaliza muda wake baada ya kudumu madarakani kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka 2015 - 2020, ni Mwenyekiti Kadama Malunde, Makamu Mwenyekiti Shaban Alley, Katibu Ali Lityawi, Mweka Hazina Stella Ibengwe, na wajumbe watano wa kamati tendaji ambao ni Marco Maduhu, Kareny Masasi, Suzy Butondo, Shija Felician na Patrick Mabula.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi, Msimamizi wa uchaguzi huo, David Nkulila alimtangaza Greyson Kakuru kuwa Mwenyekiti mpya wa Shinyanga Press Club (SPC) baada ya kuibuka na ushindi wa kura 12 dhidi ya washindani wake, Stella Ibengwe aliyepata kura 11 na Kadama Malunde aliyepata kura 10.

Pia Patrick Mabula ametangazwa kuwa Makamu Mwenyekiti baada ya kupigiwa kura za ndiyo 28, hapana 3 na moja iliyoharibika.

Vile vile, Ali Lityawi ameibuka kuwa Katibu Mtendaji wa klabu hiyo baada ya kumshinda mpinzani wake, Moshi Ndugulile, ambapo mshindi huyo alipata kura 18, huku Moshi Ndugulile akipata kura 14.

Kasisi Kosta alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi kwa kura za ndiyo 27, za hapana 4 na moja ikiharibika huku  Kareny Masasy amechaguliwa kuwa Mweka Hazina baada ya kupata kura 27 za ndiyo na tano za hapana, huku wajumbe watano wa kamati tendaji wakichaguliwa ambao ni Shija Felician, Suzy Butondo, Marco Maduhu, Marco Mipawa na Frank Mshana.

Mkutano huo wa uchaguzi ulihudhuriwa na wajumbe 33 kati ya wanachama 39 wa SPC ambapo wawili ni wagonjwa, wawili wakiwa na ruhusa na wawili hawakufika, ambapo nafasi nyingine zote zilipigiwa kura na wajumbe 32, kasoro nafasi ya Mwenyekiti ambayo ilipigiwa kura 33 baada ya mwanachama mmoja kuongezeka wakati zoezi la upigaji kura likiendelea.

Pia kabla ya zoezi la upigaji kura, wagombea wote walipewa fursa ya kujinadi kwa dakika tatu kila mmoja, huku wajumbe wakipewa fursa ya kuuliza maswali matatu kwa kila mgombea.

Akiwapongeza wanachama wenzake kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo, Mwenyekiti Mpya wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Shinyanga (SPC), Greyson Kakuru aliwashukuru wanachama kwa kumuamini na kumpa ushindi huo, huku akieleza kuwa kwa sasa safu yake inalo deni kubwa la kuyatimiza yale iliyoahidi na kwamba kila mwanachama atakuwa na nafasi sawa kukijenga chama hicho.

Naye Katibu mpya wa SPC, Ally Lityawi aliwashukuru wajumbe na kueleza kwamba sasa wanakwenda kuchapa kazi kwa kuyatimiza yale yaliyoahidiwa, kuwaunganisha waandishi, kutengeneza mahusiano mazuri na wadau na kutetea maslahi ya wanahabari mkoani hapa.

"Chama hiki ni chetu zote tushirikiane kukijenga, mimi siyo mkamilifu penye mapungufu tufuatane kushauriana," amesema.

Akizungumza na kuwashukuru wanachama, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Kadama Malunde aliwapongeza wajumbe kwa kufanya uchaguzi wa huru na haki ambao umeleta mvuto mkubwa, huku akiwahimiza waliochaguliwa kuzingatia maadili na kuacha kutoa maamuzi ya haraka yatakayowaumiza wanachama wa klabu hiyo.

"Viongozi mliochaguliwa leo hakikisheni mnazingatia katiba ya SPC na msifanye mambo kwa kukurupuka. Pia kamati tendaji isiendeshe SPC kwa chuki bali itoe fursa sawa kwa wanachama na msitengeneze makundi baina yenu, viongozi wapewe ushirikiano na wasisite kutuomba ushauri na mawazo," amesema Malunde.

Msimamizi wa uchaguzi huo, David Nkulila amesema utaratibu wote umefuatwa na hakuna malalamiko yoyote na kwamba SPC imefanikisha uchaguzi huo kwa utulivu mkubwa, ambapo amewasihi wanahabari hao kuendelea kuwa wamoja kukijenga chama chao na kuyapigania maslahi ya nchi.

Pia mkutano huo kwa kauli moja umewapitisha Stella Ibengwe, Simeo Makoba, Suleiman Abeid, David Nkulila na Hakimu Masesa kuwa wajumbe wa Kamati ya Maadili na Usuluhishi ya Klabu hiyo.
Msimamizi wa uchaguzi huo, David Nkulila akizungumza wakati wa uchaguzi wa Viongozi wa Shinyanga Press Club
Mwenyekiti Mpya wa SPC, Greyson Kakuru akizungumza baada ya kutangazwa mshindi nafasi ya mwenyekiti wa SPC
Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Kadama Malunde (kulia) akimpongeza mwenyekiti mpya wa SPC Greyson Kakuru
Wajumbe wakifuatilia mchakato wa uchaguzi
Wanachama wa SPC wakiwa ukumbini kukamilisha zoezi la uchaguzi wa klabu yao
Viongozi wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga waliomaliza muda wao (2015 - 2020) wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuvunja kamati tendaji kupisha uchaguzi wa viongozi wapya leo Julai 4,2020
Viongozi wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga waliomaliza muda wao (2015 - 2020) wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuvunja kamati tendaji kupisha uchaguzi wa viongozi wapya leo Julai 4,2020
Safu mpya ya uongozi wa SPC ikiwa katika picha ya pamoja na msimamizi wa uchaguzi huo, David Nkulila (kushoto).
Safu mpya ya uongozi wa SPC ikiwa katika picha ya pamoja
Wajumbe wakiwa ukumbini
Wajumbe wakifuatilia uchaguzi huo
Baadhi ya wanachama wa SPC wakifuatilia kwa umakini hoja za wagombea wa nafasi mbalimbali
Makamu Mwenyekiti mpya wa SPC, Patrick Mabula (kushoto)
Baadhi ya wanachama wakiwa ukumbini
Mmoja wa Wajumbe wapya wa Kamati Tendaji ya SPC, Marco Maduhu akifuatilia mchakato wa uchaguzi

Picha na Marco Maduhu na Salvatory Ntandu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com