Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mh. Anamringi Macha (kulia) akikabidhi fedha zilizookolewa kwa mmoja waWalimu wastaafu, katikati ni Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kahama ndg. Cosmas Shauri
TAARIFA KWA UMMA.
TAKUKURU KAHAMA YAOKOA SHILINGI MILIONI KUMI NA TANO ZA WALIMU WASTAAFU
NA UJENZI WA KITUO CHA AFYA NGAYA
HALMASHAURI YA WILAYA YA MSALALA.
Ofisi
ya TAKUKURU mkoa wa Shinyanga inaendelea na
uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha katika Chama cha Akiba na Mikopo cha Walimu
Kahama (WALIMU KAHAMA SACCOS LTD). Fedha hizi kiasi cha Sh. 7,780,625/=
zilizookolewa zitalipwa moja kwa moja kwa Walimu Wastaafu wanaokidai Chama Cha
Akiba na Mikopo cha Walimu Kahama (WALIMU KAHAMA SACCOS LTD) na Mhe. Mkuu wa
Wilaya ya Kahama, Mhe. Anamringi Macha.
Aidha
katika uchunguzi uliofanyika kuhusiana na ujenzi wa Kituo cha Afya cha NGAYA
kilichopo kata ya NGAYA Halmashauri ya Msalala, Ofisi ya TAKUKURU (W) Kahama
imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi
7,275,500/= ambazo zitakabidhiwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha kwa Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya MSALALA Ndugu. Simon Berege.
Kwa
hiyo jumla ya fedha zilizookolewa na ambazo zitalipwa kwa walimu wastaafu na
kukabidhiwa Halmashauri (W) Msalala ni sh.
15,056,125.00.
DENI LA WALIMU WASTAAFU.
Uchunguzi
uliofanyika na TAKUKURU mkoa wa Shinyanga kwa
WALIMU KAHAMA SACCOS LTD umebaini kwamba chama hiki kinadaiwa na walimu
wastaafu ishirini na tisa (29) jumla
ya sh. 13,396,425.00. Deni hili
linatokana na akiba za walimu wastaafu walizokuwa wanachangia wakati wakiwa
kazini baada ya kustaafu akiba hizi hazikuweza kupatikana kwa kuwa chama
kilikuwa hakina fedha.
Awamu
ya kwanza ofisi ya TAKUKURU (W) Kahama iliokoa jumla ya sh. 5,815,800.00, fedha
hizi zililipwa kwa walimu wastaafu kumi na tatu (13) waliokuwa wanakidai Chama cha Akiba na Mikopo cha Walimu
Kahama SACCOS.
Katika
awamu hii ya pili Ofisi ya TAKUKURU (W) Kahama imefanikiwa kuokoa kiasi cha sh. 7,780,625.00 fedha ambazo zitalipwa
kwa walimu wastaafu kumi na sita (16) waliosalia
ambao walikuwa wnanchama wa WALIMU KAHAMA SACCOS LTD.
FEDHA ZA UJENZI WA KITUO CHA AFYA NGAYA
ZILIZOOKOLEWA SH. 7,275,500/=
TAKUKURU
Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ilifanya
uchunguzi kuhusiana na ujenzi wa Kituo cha Afya cha NGAYA kilichoko kata ya
NGAYA Halmashauri ya Msalala ambapo katika
uchunguzi huo ilibainika kuwa kiasi cha sh.
7,275,500/= kimepotea kutokana na Mtaalamu kitengo cha manunuzi
kutotekeleza majukumu yake ipasavyo; hivyo ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Kahama
kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, imefanikiwa
kuokoa fedha hizo. Kwa kuwa kuna kazi ambazo hazijakamilika za ujenzi wa
zahanati hiyo, fedha hizo zitakabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Msalala.
WITO.
TAKUKURU
(M) SHINYANGA inatoa wito kwa watumishi wa umma mkoani
humu kufanya kazi kwa weledi, uadilifu, uzalendo, uaminifu na kwa
kufuata sheria zote za nchi ili fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya
utekelezaji wa shughuli mbali mbali zitumike kama ilivyokusudiwa. Iwapo mtumishi wa umma (mtaalam) atashindwa
kuwajibika ipasavyo na hivyo kusababisha upotevu wa fedha ya Serikali mtumishi
huyo atarejesha fedha iliyopotea na hatua nyingine za kisheria zitafuata
ikiwemo ya kumfikisha mahakamani.
Aidha
TAKUKURU mkoa wa Shinyanga inatoa wito kwa
Watumishi wa Umama mkoani humu kufichua vitendo
vya rushwa vinavyotokea katika maeneo yao ya kazi. Wapo watumishi wananwake
ambao wanaombwa rushwa ya ngono ili waweze kupatiwa upendeleo mfano kupandishwa
cheo, kupatiwa uhamisho, kupatiwa ruhusa ya kwenda masomoni na huduma nyingine
zinazofanana na hizo. TAKUKURU (M) SHINYANGA inatoa wito kwa watumishi
wanaokutana na vitendo hivi kutoa taarifa ili wahusika wachukuliwe hatua mara
moja.
Imetolewa leo tarehe
02/07/2020 na Mkuu wa TAKUKURU (W) Kahama Kwa Niaba ya Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa
Shinyanga.
Social Plugin