Viongozi wa mikoa mitano ya Chama cha ACT Wazalendo, wamemwomba Bernard Membe, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Tanzania, akubali ombi lao la kujiunga na chama hicho.
Viongozi hao ni: Mwenyekiti wa ACT Mkoa wa Lindi na mjumbe wa Kamati Kuu, Isihaka Mchinjita; Mwenyekiti wa ACT Mkoa wa Mtwara, Alphonce Hitu; Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kichama Selous, na Abdallah Mtalika; na Mwenyekiti wa ACT Mkoa wa Pwani, Mrisho Swagara.
Kwa mujibu wa tamko hilo, viongozi hao walikwenda Kijiji cha Rondo kuwasilisha ombi maalum kwa Membe kujiunga na chama chao.
Walikumbusha kwamba Juni 30, mwaka huu,wakati Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, akihutubia wanachama katika mkutano wa ndani uliofanyika Kilwa Kivinje mkoani Lindi, alimwalika Membe kujiunga na vyama vya upinzani, ili kuongeza mshikamano kuhami demokrasia na kuleta mabadiliko ya utawala nchini.
“Kwetu wito huu ulikuwa ni hatua muhimu kuelekea mageuzi makubwa ya kisiasa nchini. Uamuzi wa Membe wa kurudisha kadi ya CCM tumeupokea kwa matarajio makubwa.
“Hii ni kwa sababu uamuzi huu unafungua milango kwa yeye kuchagua kujiunga na vyama vya siasa vya upinzani nchini ikiwa ataona inafaa," ilielezwa katika tamko lao hilo.
Viongozi hao walisema wamekuwa wakifuatilia kwa umakini misimamo, mwelekeo na mitazamo ya Membe kuhusu demokrasia, haki na utawala wa sheria.
“Kwa hakika, tunaamini kuwa hayo ndiyo yaliyokufanya ufukuzwe CCM. Hata hivyo, mambo haya uliyoyapigania ukiwa ndani ya CCM ni hitaji kubwa la taifa letu, ndiyo maana sisi viongozi tumekuja hapa kukuomba ujiunge na chama chetu cha ACT-Wazalendo. " walieleza katika tamko lao hilo.
Social Plugin