Wafanyabiasahara wawili wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka saba ikiwamo kukwepa kodi na kutakatisha Sh. bilioni 5.5.
Washtakiwa hao ni Ike Godfrey maarufu kama Maliki (30), mkazi wa Tabata Segerea na Abdi Mussa, ambao walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, akisaidiana na Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto, alidai kuwa washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Julai 13, 2019 na Aprili 16, 2020 maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, walikula njama kutenda kosa la kukwepa kodi.
Wankyo alidai Mei 5, 2019 maeneo ya Dar es Salaam mshtakiwa Maliki alighushi saini ya Mohamood Warsame, lengo likiwa ni kuonyesha kuwa saini hiyo ni halisi na ni ya Warsame wakati akijua sio kweli.
Pia alidai katika tarehe hiyo, Maliki akiwa na lengo la kughushi, alijitambulisha kwa Faustina Seki, kuwa yeye ni Warsame jambo ambalo si kweli.
Katika shtaka ya nne, Simon alidai Julai 13, 2019 na Aprili 16, 2020 maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, Mussa kwa lengo la kukwepa kodi alitumia mashine ya kielektroniki ya EFD ambazo hazijasajiliwa kwa jina lake na hivyo kukwepa kodi ya Sh. 136,947,481 iliyopaswa kulipwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Ilidaiwa kuwa katika tarehe hizo, Mussa alishindwa kulipa kodi ya Sh. 5,397,431,501 na katika shtaka la sita mshtakiwa Mussa anadaiwa kwa kutumia mashine ya EFD isiyosajiliwa na jina lake, alisababisha hasara ya Sh. 5,571,205,189.
Katika shtaka la saba, Wakili Mitanto alidai Julai 13, 2019 na Aprili 16, 2020 maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu Maliki alitumia mashine hizo na kusababisha hasara ya Sh. 5,571,205,189.
Pia alidai washtakiwa hao walijipatia Sh. 5,571,205,189 wakati wakijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu kutokana na kukwepa kodi.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.
Upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo, aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa walirudishwa rumande mpaka Agosti 12, mwaka huu kwa kuwa mashtaka hayo hayana dhamana.