Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAGOMBEA 19 CCM KILOSA NA 20 MIKUMI WAJITOKEZA KUCHUKUA FOMU ZA UBUNGE


Jumla ya wanachama 19 wa Chama Cha Mapinduzi katika jimbo la Kilosa wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea Ubunge katika jimbo hilo ikiwa ni siku ya kwanza tu tangu zoezi la uchukuaji fomu kupitia CCM lianze rasmi.



Mmoja wa watu waliojitokeza kuchukua fomu za kugombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi katika jimbo la Kilosa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ambae mara baada ya kuchukua fomu hiyo amesema baada ya kulitumikia taifa kwa ujumla kupitia taaluma yake sasa ni wakati wa kushirikiana na wananchi wa Jimbo la Kilosa Mkoani Morogoro ili kutatua changamoto zinazowakabili kutokana na uzoefu wa kiutendaji alioupata.

Ameongeza kuwa hakwenda jimboni humo kutafuta umaarufu bali amekwenda kwa ajili ya kuitumia taaluma na uzoefu wake kwa kushirikiana na wananchi wa eneo alikozaliwa na kukulia ili kutatua changamoto mbalimbali hususani migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikisababisha mauaji pia kulifanya jimbo hilo kuwa eneo la kimkakati kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara na kuhamasisha uwekezaji ambao utatatua changamoto nyingine ikiwemo maji na barabara.

Kaimu Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kilosa Bw Filbert Kapenda amesema mwamko wa uchukuaji fomu za kugombea nafasi ya Ubunge kwa jimbo hilo la Kilosa ni kubwa na kwamba kwa hii leo pekee jumla ya wanachama 19 wamejitokeza kuchukua fomu kwa jimbo la Kilosa pekee huku jimbo la Mikumi wakiwa wamejitokeza wanachama 20.

Pazia la uchukuaji fomu kwa ajili ya kugombea nafasi za udiwani na ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi kwa Tanzania Bara pamoja na Zanzibar kwa kiti cha uwakilishi limefunguliwa hii leo na linatarajiwa kuhitimishwa Julai 17,2020.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com