Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKAMATWA KWA KUWAFUNDISHA WATOTO WADOGO NGONO

Na Mwandishi Wetu,Tunduru
JUMLA ya  wazazi 35 kutoka kata ya Nalasi wilayani Tunduru wamekatwa  baada ya kukukutwa wakiwafundisha watoto wa kike walio chini ya umri wa miaka 8  mbinu za kuishi na wanaume  na kufanya tendo la ngono maarufu kama msondo.


Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo alisema, wazazi hao wamekamatwa  nyakati za usiku wakiwa wamejifungia kwenye  nyumba mmoja wa waliokamatwa  katika kijiji cha Nalasi wakiwa na watoto hao.

Alisema, wazazi hao wamekamatwa  baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kwamba,kuna wazazi  wamewaficha watoto wa kike wenye umri mdogo na kuwafundisha mila potofu zinazohusiana na mambo ya ngono ambayo hayapaswi kufundishwa watoto wadogo.

Mtatiro alisema, wazazi hao walikamatwa nyakati za usiku wakiwa na watoto hao wadogo  wakiwa katika moja ya nyumba iliyokuwa inatumika  kwa shughuli hiyo.

Pia alisema,katika msako huo mbali na wazazi hao wamemkamata Kungwi mmoja,mtendaji wa Rajabu Lusanga na mwenyekiti wa kijiji cha Nalasi Ali Omari ambao wameshindwa kuchukua hatua dhidi ya wazazi hao licha ya kuishi jirani na eneo la tukio hilo.

Kwa mujibu wake shughuli za msondo hazikatwi kufanywa, isipokuwa ni kwa wasichana wakubwa wenye umri zaidi ya miaka 18 na wale wanatarajia kuolewa, badala ya kuwafundisha watoto wadogo ambao hawana uwezo wa  kuelewa jambo lolote.

“natoa wito kwa wazazi wote katika wilaya ya Tunduru tabia ya kuwafundisha watoto wadogo namna ya kuishi mama na baba jambo hilo tumelipiga marufuku kwani linachangia sana kuongezeka kwa mimba na wasichana wengi kuacha shule”alisema, Mtatiro.

Alisema, vitendo hivyo vinasababisha watoto wadogo wa kike kukosa haki yao ya kupata elimu na kusisitiza kuwa operesheni hiyo itaendelea katika vijiji mbalimbali hadi pale jamii itakapo acha  kufanya vitendo hivyo.

Baadhi ya wakazi wa Tunduru wamepongeza jitihada kubwa zinazo fanywa na Serikali ikiongozwa na Mkuu wa wilaya ya kukomesha baadhi ya mira potofu ambazo zimekuwa chanzo cha kuongezeka kwa mimba kwa watoto wa kike wengine  kuacha masomo.

Ali Shaibu mkazi wa Nakayaya alisema,jitihada zinazofanywa na Dc Mtatiro zinapaswa kuungwa mkono na jamii ya watu wa Tunduru kwani zitasaidia kuepusha mimba za utotoni,kupata  magonjwa mbalimbali ikiwemo ukimwi na kupoteza vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya familia na Taifa.

Awetu Rashid, ameiomba Serikali kuendelea kuchukua hatua ya kukomesha vitendo hivyo ambavyo kwa muda mrefu vimechangia wilaya hiyo kubaki nyuma kielimu na hivyo kuwa maskini licha ya ukweli kwamba imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com