Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAWAKE NA HAKI YA KUTOA MAONI NA KUPATA TAARIFA: CHANGAMOTO NA FAIDA ZAKE



Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Wanawake na wasichana wamekuwa wahanga wakuu wa ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu ikiwemo haki ya kupata taarifa na kutoa mawazo yao. 

Kwa mujibu wa Shirika la Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa haki ya kupata taarifa na kutoa maoni kwa wanawake wengi barani Afrika.

 Ingawa kundi hili huwakilisha idadi kubwa ya watu wote wa bara hili na takriban asilimia 55 ya Watanzania wote bado sauti za wanawake wengi hazisikiki katika mijadala na majukwaa mbalimbali. 

Ingawa Tanzania ni miongozi mwa nchi za Kusini mwa Afrika zenye idadi kubwa ya vyombo vya habari (vituo 183 vya redio, vituo takribani 50 vya Runinga/TV) bado havijatoa fursa za kutosha kwa sauti za wanawake katika maudhui mbalimbali yanayoandaliwa.

 Hali ni mbaya zaidi kwa wanawake wanaoishi vijijini ambao, pamoja na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii wanazokumbana nazo, bado wanashindwa kupaza sauti zao kueleza masahibu wanayokumbana nayo.


Changamoto zinazokwamisha haki ya Mwanamke kupata na kutoa Taarifa:

Changamoto mbalimbali zinazomkwamisha mwanamke nchini katika kueleza hisia na kuwasilisha mawazo yake kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari ni pamoja na mila na desturi potofu, fursa chache za kushiriki katika mijadala ya vyombo vya habari, hofu ya kushiriki katika maudhui yanayoandaliwa na vyombo vya habari.

Mila na desturi potofu za baadhi ya makabila zinamnyima mwanamke hasa wa vijijini haki ya kuchangia mawazo yake katika majukwaa kama vikao vya familia, mikutano ya kijiji/mtaa, maeneo ya kazi, na mijadala ya kimaamuzi. 

Kwa kiasi kikubwa mila na desturi hizi zinambagua mwanamke na kumuona ni mtu asiye na uwezo na mchango wowote.

 Mila na desturi hizi zimeathiri kwa kiasi kikubwa saikolojia ya wanawake walio wengi ikiwemo kutojiamini na kuwa na hofu ya kueleza kile wanachokiamini pale zinapopatikana fursa za kushiriki katika majadiliano na/au mahojiano na vyombo vya habari. 


Aidha, uwepo wa idadi kubwa (takriban asilimia 65) ya waandishi wa habari na wale wanaofanya maamuzi ya kihabari katika vyombo vya habari ni wanaume na hivyo kuathiri maudhui mengi yenye sauti za wanaume zaidi kuliko sauti za wanawake.

 Changamoto hii kwa wanawake ipo katika maeneo mengine yakiwemo kukosa ujasiri wa kugombea uongozi. 


Kikwazo kingine kinachodumaza haki ya wanawake, hususan wale waishio vijijini, kutoa mawazo yao ni fursa finyu ya kushiriki kwenye maudhui na mijadala ya vyombo vya habari.

 Ingawa Tanzania ina idadi kubwa ya vyombo vya habari zikiwemo redio jamii, bado havijasambaa maeneo mengi ya vijijini. 

Aidha, vyombo hivi huendeshwa kibiashara na hivyo kutoa nafasi finyu kwa sauti za wanawake zisizokidhi malengo yao ya kibiashara.

 Hivyo, mawazo ya wanawake wa hali ya chini na waishio vijijini hayasikiki au kupewa kipaumbele kwenye vyombo vya habari.

 Sauti za wanawake zinazosikika katika majukwaa mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari zinawakisha wanawake wasomi na waliofanikiwa kibiashara au kitaaluma. Bahati mbaya, sauti hizi haziakisi mawazo na masuala ya msingi ya wanawake walio wengi. 


Wajibu wa vyombo vya habari:


Vyombo vya habari vina wajibu wa kuwajengea uwezo wanawake ili wajiamini na kutoa mawazo yao kwa kushiriki katika mijadala mbalimbali ya kihabari.

 Hii ni pamoja na kuendesha kampeni dhidi ya mila na desturi potofu zinazowazuia wanawake kutoa mawazo katika ngazi za maamuzi na kupaza sauti zao kuhusu masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. 


Maudhui yanayoandaliwa yahusishe sauti za wanawake ili kutoa fursa kwao kupaza sauti zao kwa kushiriki kikamilifu katika mijadala na kuchangia mawazo yao. 

Vyombo vya habari vifanye marekebisho ya sera ya vyombo vyao ili kuhakikisha maudhui yote yanakuwa na ulinganifu wa sauti za wanawake na wanaume.


Taasisi za kihabari, mfano MISA Tanzania, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari (UTPC) na vyuo vya uandishi wa habari (SJMC, Tumaini, DSJ, n.k.) nchini viendeshe mafunzo ya kuwajengea uwezo na kujiamini wanawake ili waweze kutoa mawazo yao kupitia majukwaa mbalimbali hususan vyombo vya habari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com