Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage Akizungumza na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ambao ndio wasimamizi wakuu wa uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu.
Wakurugenzi wa Halmashauri ambao ndio wasimamizi wa uchaguzi mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani wakiwa kwenye mkutano na Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ya awali ya uchaguzi huo.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC) Dk Wilson Charles Mahera akizungumza katika mkutano wa pamoja na wasimamizi wa uchaguzi mkuu ujao.
Charles James, Michuzi TV
TUME ya Uchaguzi (NEC) imewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini ambao ndio wasimamizi wa uchaguzi mkuu ujao kuzingatia maadili na kanuni za uchaguzi kama zinavyoelekeza.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage wakati wa kufungua mafunzo ya awali ya siku moja kwa Wakurugenzi hao leo jijini Dodoma.
Jaji Kaijage amewapongeza wakurugenzi hao kwa kuteuliwa kuwa wasimamizi wakuu wa uchaguzi na kuwaeleza kuwa wana jukumu kubwa la kusimamia uchaguzi huo ili uweze kufanyika kwa uwazi na wenye haki.
Amewataka kuandaa mpango mzuri wa uchaguzi huo kwa kufanya tathmini ya kujua maeneo yao kwa kuangalia Jiografia yenyewe, hali ya usafiri pamoja na hali ya kisiasa ili kuepuka athari za uchaguzi.
Kuhusu fedha za uchaguzi Jaji Kaijage amesema tayari wasimamizi hao washaingiziwa fedha za awali kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi huo na awamu ya pili na tatu ya fedha hizo zipo kwenye mchakato na muda siyo mrefu wataingiziwa kwenye akaunti zao.
" Niwapongeze kwa kuaminiwa kuwa wasimamizi wa uchaguzi huu wa Rais, Wabunge na Madiwani, nyie mna dhamana kubwa kwenye uchaguzi huu, niwatake mkasimamie kwa uadilifu, uzalendo huku mkifuata maadili na kanuni za uchaguzi.
Tayari fedha za uchaguzi awamu ya kwanza tumeshawaingizia, niwasihi mkazitumie vizuri kwa kuzingatia sheria za fedha, kuhusu vifaa tayari vishakufa na vingine viko njiani, nitoe rai kwenu kuviweka kwenye mazingira mazuri kuelekea uchaguzi, " Amesema Jaji Kaijage.
Jaji Kaijage amesema wanatarajia kuwepo kwa waangalizi wa uchaguzi kutoka Nje ya Nchi na tayari wanawasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje ili kujua wasimamizi watakaokuja na watapatiwa vibali maalum pamoja na watazamaji wa ndani ya Nchi.
Amesema pia wametoa kibali kwa Asasi zisizo za kiraia 245 Tanzania Bara na Saba kutoka Zanzibar kwa ajili ya kutoa elimu ya uchaguzi kwa wananchi na kuwataka wasimamizi hao kuwapa ushirikiano huku wakihakikisha hawavunji kanuni.
Social Plugin