Wawekezaji wa ndani ya nchi wamehamasishwa kujitokeza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya mbolea hapa nchini ili kusaidia upatikanaji wa mbolea bora na yenye gharama nafuu kwa wakulima.
Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ametoa wito huo jana (11.07.2020) wakati wa ziara yake ya kikazi wilaya ya Mufindi mkoa wa Iringa kujionea hali ya uzalishaji mazao ya pareto na chai.
Kusaya alisema kuwa hali ya uzalishaji mazao hayo umekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka kutokana na malalamiko ya wakulima kushindwa kumudu gharama ya bei kubwa ya pembejeo na mbolea.
“Nitafurahi zaidi nikisikia watanzania wanaanzisha uwekezaji katika viwanda vya mbolea ili tusaidie wakulima wetu kwani kwa sasa katika baadhi ya maeneo wakulima wengi wanashindwa kununua mbolea mfuko wa kilo 50 kwa shilingi 90,000 “ alisema Kusaya
Akiwa kijiji cha Mkonge wilaya ya Mufindi Katibu Mkuu huyo alipokea malalamiko ya wakulima wadogo wa chai kuwa chai yao inakataliwa na wenye viwanda kwa madai kuwa ina ubora mdogo uliosababishwa na kutumia mbolea yenye ubora mdogo .
Wakulima hao wa chama cha ushirika cha wakulima wa chai Mkonge wanadai kukopeshwa mbolea na kampuni ya Uniliver ya Mufindi ambayo pia ni mmoja wa wanunuzi wanaokataa kununua majani mabichi ya wakulima hao na kusababisha hasara kwa wakulima.
“ Chai tulipeleka mwaka huu kiwandani Uniliver tukaambiwa haina ubora kisha wakaimwaga kwa kuwa tulitumia mbolea ya minjingu isiyo na ubora,hii hasara nani atatulipa “ alisema Jimson Sigala mkulima wa chai
Katibu Mkuu huyo aliongeza kusema wizara ya kilimo inahitaji mkulima atumie mbolea itakayoongeza tija katika uzalishaji hivyo amewasihi watanzania kujitokeza kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda ndani ya nchi na kuwa serikali ya Awamu ya tano itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.
Kwa mujibu wa Wakala wa Udhibiti wa Mbolea (TFRA) hali ya upatikanaji wa mbolea nchini imeongezeka kutoka tani 302,482 mwaka 2015/2016 hadi tani 604,978 mwaka 2019/2020 hata hivyo mahitaji bado ni makubwa sana kwani mbolea nyingi zinaagizwa nje ya nchi na kuwa bei kubwa.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Kusaya amewasihi wakulima wa chai Mufindi na kote nchini kutumia Kituo cha Utafiti wa zao la Chai ( TRIT) kupata huduma za ushauri ili waongeze tija katika uzalishaji wa zao la chai nchini.
“ Wakulima nendeni kwenye kituo chetu cha Utafiti TRIT kupata elimu juu ya kilimo cha chai ikiwemo kupata huduma ya upimaji afya ya udongo kujua aina ya virutubishi na mbolea inayotakiwa kuongeza uzalishaji na kuwezesha mkulima anufaike na kilimo” Kusaya alisisitiza
Wakulima wadogo wa chai Mufindi waliomba serikali iwasaidie kupata bei nzuri ya chai kwani bei ya sasa ni ndogo na haiendani na gharama za uzalishaji.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima Abeid Mhongole mkazi wa Luhunga Mufindi alisema bei ya shilingi 314 kwa kilo moja ya majani ya chai haileti manufaa kwa wakulima na zaidi inawakatisha tamaa kuendelea kuzalisha zao la chai.
Akijibu kero hiyo Katibu Mkuu Kusaya alisema atakutana na Katibu Mkuu wizara ya Viwanda na Biashara Prof.Riziki Shemdoe hivi karibuni kujadili namna ya kupata ufumbuzi wa malalamiko ya bei ya zao la chai na kuwa ikibidi wasaidie kupatikana kiwanda cha chai kwa wakulima wadogo.
Aidha Kusaya aliwataka viongozi wa chama hicho cha ushirika kuwasilisha maombi yao ya kupta mtaji katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili waweze kupata uwezo wa kununua mbolea bora moja kwa moja toka kwenye viwanda badala ya kupitia mawakala.
“ Tukiwa na bei nzuri ya zao la chai, tutawavutia vijana wengi kulima na kuondoa utegemezi wa wazee kuendeleza kuzalisha zao hili muhimu kwa uchumi wa nchi” alisema Kusaya
Mwisho
Imetolewa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
Makambako
12.07.2020
Social Plugin