Na.Angela Msimbira ARUSHA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Mhe. Selemani Jafo amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Mhandisi Victor Seif kumuhamisha mara moja aliyekuwa Meneja wa Tarura Jiji la Arusha na kumpangia kazi nyingine ya kiwango cha chini.
Ametoa maagizo hayo jana wakati alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua Miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Mkoani Arusha
Mhe. Jafo alisema ameamua kumuhamisha Mtumishi huyo kutokana na kutokutoa taarifa za miradi ya maendeleo yanayofanywa na Serikali , jambo ambalo linasabisha Serikali ionekane inashindwa kutimiza majukumu yake ya kuleta maendeleo kwa wananchi
Amewaagiza watendaji wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo na kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili wananchi waweze kuijua na kutambua kuwa miradi hiyo imefanywa na Serikali
“Watendaji wote nchini mnawajibu wa kuhakikisha mnasimamia miradi ya Maendeleo kwa weledi mkubwa ili iweze kukamilika kwa wakati na kuitangaza kwa wananchi ili iweze kuijua, kuitunza na kuithamini miradi hiyo.” Amesisitiza Mhe. Jafo
Aidha Mhe. Jafo amewaagiza watendaji wote nchini ambao wamepewa dhamana ya kuwahudumia wananchi watimize majukumu yao kikamilifu ili kutatua kero za wananchi kwa wakati na kuleta maendeleo kwa jamii.
Social Plugin