Waziri Mkuu wa Ivory Coast, Amadou Gon Coulibaly, amefariki dunia ghafla usiku wa kuamkia leo Alhamisi akiwa na umri wa miaka 61.
Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kumnukuu Rais Alassane Ouattara wa Kodivaa akitangaza jana usiku kwamba Ivory Coast imeingia kwenye msiba wa kuondokewa ghafla na Coulibaly.
Aidha amesema, Waziri Mkuu Coulibaly alishiriki kwenye kikao cha kila wiki cha Baraza la Mawaziri la serikali ya Kodivaa, hali yake ikawa mbaya na amefariki dunia hospitalini.
Mwezi Machi mwaka huu, Coulibaly aliteuliwa na chama tawala wa Ivory Coast kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho ili kumrithi Rais Alassane Ouattara.
Waziri Mkuu huyo alirejea nchini Kodivaa tarehe pili mwezi huu wa Julai baada ya kupitisha muda mrefu wa matibabu nchini Ufaransa. Aliwahi kufanyiwa operesheni ya moyo mwaka 2012.
Ouattara amemtaja Colibaly kwamba alikuwa mtu wake wake wa karibu mno katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Haikuweza kujulikana haraka ni nani atateuliwa kushika nafasi yake ya kugombea urais wa tiketi ya chama tawala katika nchi hiyo ambayo ni mzalishaji mkubwa wa cocoa duniani.
Social Plugin