Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba akiangalia gari dogo aina ya Toyota Secced baada ya kugongana na basi dogo aina ya TATA, mali ya Kampuni ya NBS lililokuwa likitoka jijini Mwanza kuelekea mkoani Tabora
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Watu watano wamefariki dunia papo hapo katika ajali iliyohusisha gari ndogo lililogongana na basi dogo la Kampuni ya NBS katika kijiji cha Nyasamba wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga barabara ya Shinyanga - Mwanza leo Alhamis Agosti 27,2020.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba ambaye amefika eneo la tukio amesema chanzo cha ajali hiyo ni gari dogo aina ya Toyota Secced kukosa mwelekeo na kugonga basi dogo aina ya TATA, mali ya Kampuni ya NBS lililokuwa likitoka jijini Mwanza kuelekea mkoani Tabora.
"Gari lenye namba za usajili T571 BPZ aina ya Tata Mini Bus ikiendeshwa na Kazimili Maganga likitokea Mwanza kwenda Tabora lilipofika eneo la Nyasamba liligongana na gari jingine dogo likitokea Dar es salaam likiendeshwa na Ramadhan Silaji na kusababisha vifo vya watu watano",ameeleza Kamanda Magiligimba.
"Chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa madereva wa magari yote mawili na uzembe wa dereva dogo ambapo alihama upande wa kushoto na kuendeshea kulia zaidi na kwenda kugongana na basi hilo dogo na kusababisha vifo vya watu watano",amesema Kamanda Magiligimba.
Amewataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Ramadhan Silaji, Godfrey Gaspar,Anthony Pastory,Mallya Wambura na Abdul Juma na kwamba Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, waliozungumza na Malunde 1 blog wamesema baada ya ajali kutokea gari ndogo iliburuzwa na basi huku wakieleza kuwa dereva wa gari dogo alikuwa anaendesha kwa mwendokasi,ikapasua tairi na kugongana na basi na kusababisha vifo vya watu watano waliokuwa ndani ya gari dogo.Muonekano wa basi la NBS na gari ndogo baada ya kupata ajali leo Alhamis Agosti 27,2020. Picha na Malunde 1 blog
Muonekano wa gari dogo aina ya Toyota Secced na basi dogo aina ya TATA, mali ya Kampuni ya NBS baada ya ajali kutokea
Social Plugin