Mfano wa Basi la shule
Na Abby Nkungu, Singida
TATIZO la wanafunzi shule za mchepuo wa Kiingereza (English Medium) kuchelewa kuchukuliwa kwenda shuleni na kurejeshwa nyumbani katika Manispaa ya Singida sasa limebaki historia baada ya Serikali kuchukua hatua mbalimbali; ikiwemo kuwataka wamiliki wa Taasisi hizo kuwa na mabasi ya kutosha.
Mwandishi wa habari hizi amebaini kuwa baada ya janga la Corona kupungua na shule kufunguliwa, Serikali iliwahimiza wamiliki wa shule hizo kuwa na mabasi ya kutosha kuepuka msongamano wa watoto wanapokwenda shuleni na kurejea nyumbani ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia kusambaa zaidi kwa maambukizi ya virusi vya COVID-19.
Awali, baadhi ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma kutwa katika shule hizo walilalamika kwenye majukwaa mbalimbali watoto wao kulazimika kuamka saa 11:00 alfajiri kila siku za masomo kwa ajili ya kujiandaa kwenda shule na kuchelewa kurejea nyumbani hadi saa 2:00 usiku.
Walisema kuwa hali hiyo ilikuwa ikileta adha kubwa kwa mtoto wa shule za awali mwenye umri wa chini ya miaka sita kulazimika kuamka mapema alfajiri na kurejea usiku; hivyo kuchoka na kusababisha achukie shule kwa kuona kama vile ni adhabu.
Ilielezwa kuwa moja ya sababu kuu iliyochangia watoto wao kuamka mapema ni uhaba wa mabasi ya shule hizo; hivyo gari moja kulazimika kuanza mzunguko wa kuwachukua watoto mapema alfajiri kuwapeleka shule ili kurudi kuchukua wengine. Vivyo hivyo, wakati wa kuwarejesha nyumbani jioni.
“Tunashukuru Mungu baada ya kupiga kelele kupitia vyombo vya habari, Serikali ikasikia na kuwabana wamiliki wa shule. Wengi wao wameongeza magari sasa mtoto anaweza kuamka saa moja akajiandaa na kurejeshwa saa 11 jioni” alisema Halima Njiku mkazi wa Kibaoni mjini Singida.
“Janga la Corona limetusaidia sana, watoto hawapakatiani tena kwenye viti kwani shule nyingi zimeongeza magari kuepuka kufungiwa; hivyo kilio chetu cha muda mrefu kupitia vyombo vya habari kimesikika...tunashukuru” alisema mzazi mwingine, Juma Omari mkazi wa Mwenge mjini hapa.
Ofisa elimu Taaluma shule za Msingi Manispaa ya Singida, Gerson Mrua alisema baada ya malalamiko ya wazazi na walezi, waliamua kuwaandikia barua wamiliki wote wa shule hizo za English Medium kuwataka wawe na magari ya kutosha kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma kutwa.
“Lakini pia tuliwaagiza warekebishe ratiba zao za kuwachukua asubuhi na kuwarejesha jioni wanafunzi ili kupunguza adha kwa wazazi, walezi na watoto pia" alisema Ofisa huyo.
Wataalam wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto wanasema mtoto anapaswa kupumzika angalau kwa saa moja hadi mbili awapo shuleni na kwa shule zinazokaa na watoto kwa muda mrefu zaidi lazima ziwe na ratiba yenye huduma ya mapumziko; ikiwemo kulala kwa muda kwa kuwa kupumzika ni afya kwa mtoto kwani ubongo wake bado unakua kwa kasi. MWISHO