Mtia nia kugombea Ubunge Jimbo la Busanda Simon Bigambo Chozaile
Katika hali inayoonesha kuchukizwa na kauli zinazoendelea kutolewa dhidi ya Wajumbe wa CCM katika Uchaguzi wa kura za maoni kwenye mchakato wa kupata wagombea Ubunge na udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi, Kada wa CCM Simon Bigambo Chozaile ambaye naye alijitosa katika mchakato wa kuomba chama chake kimchague kuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Usanda ameandika waraka ufuatao:
WAJUMBE KUTUKANWA, KUSEMWA VIBAYA NA KUONDOLEWA UTU WAO
Tangu tarehe 20/7/2020 na 21/7/2020 pamekuwepo kauli tofauti tofauti kutoka kwa Wagombea wengi wa Chama chetu Cha Mapinduzi (CCM) hasa wale ambao kura zao hazikutosha wakionesha kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Jimbo sio watu wazuri kwa sababu hawakuwapigia kura.
Ninaomba kutumia fursa hii kusema mambo machache kuhusu hili;
Kwanza wagombea hawa wameshindwa kujua kikao hiki kina uzito gani na kwamba kugombea kwao hakungebadili maoni ya wajumbe wa mkutano wa Jimbo.
Wanatakiwa watambue kuwa Wajumbe wanayo haki kikatiba kuchagua kiongozi ambaye wanampenda na wangependa awaongoze.
Wajumbe ni watu wazima na kwamba wanayo maamuzi yao na maamuzi yao ni Siri yao kwa hiyo hata wakicheka na wewe bado wanayo maamuzi ya ama kukuchagua au kutokukuchagua.
Hivyo naomba wagombea wenzangu ambao kura zetu hazikutosha tuwaheshimu viongozi wetu wa Chama yaani Mwenyekiti wa CCM wilaya, Wenyeviti wa CCM kata zote zilizounda Jimbo ulilogombea, makatibu wa CCM na makatibu waenezi wa kata zote.
Viongozi wa Jumuiya zote ngazi za kata yaani Wazazi, UWT na UVCCM ngazi za kata na matawi. Hawa ni viongozi bwa CCM katika ngazi zao wa wanastahili heshima.
USHAURI WANGU KWA WAGOMBEA
Kwanza kutambua mkutano wa Jimbo ni mkutano ambao unatoa maoni ya muhimu kabisa katika hatua za upembuzi wa nani apeperushe bendera ya CCM katika Jimbo husika.
Wagombea wawaheshimu wajumbe (viongozi wa CCM ngazi ya Jimbo) kwani kushindwa kwao kusiondoe utu wa viongozi wetu.
Ndugu zangu wagombea ni lazima mkubali kuwa hata kama tungekuwa wawili bado mshindi alitakiwa mmoja.
Hivyo kauli zenu zinaingilia vikao vya juu zaidi katika kufanya maamuzi yake.
Naamini wote wanaotumia kauli hii wengi sio wazalendo na walikwenda na majibu ya Uchaguzi mifukoni.
Pili wengi ni wasanii, wahuni na wasiojua mipaka na kanuni za chama chetu pamoja na utendaji wake.
Mwisho ninawaomba wasiendelee kutumia lugha chafu, lugha za kejeli na matusi na zenye kuondoa utu wa viongozi hawa wa Chama katika ngazi husika.Hawa ni viongozi wa Chama na maoni yao yaheshimiwe na matarajio ya kugombea kwetu yasiondoe utu wao. Naomba tuwe na kiasi na nidhamu kwa viongozi wetu.
Imetolewa na Simon Bigambo Chozaile (0674101933)
Mgombea Ubunge CCM Jimbo la BUSANDA
Simon Bigambo Chozaile akichukua fomu kugombea ubunge Jimbo la Busanda mwezi Julai 2020