Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Mpango akipokea mfano wa hundi ya gawio la shilingi bilioni 9.3 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (watatu kushoto) kutokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya benki hiyo kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa DANIDA kwa kushirikiana na Serikali ya Denmark. Waziri Mpango leo amepokea jumla ya gawio la shilingi bilioni 17 kutoka Benki ya CRDB ikiwa ni gawio kutokana na uwekezaji wa Serikali kuu, taasisi na mashirika yake. Wengine pichani ni Waziri wa TAMISEMI, Suleiman Jaffo (wanne kushoto), Waziri wa Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (watatu kulia), Balozi wa Denmark Nchini, Mette Dissing-Spandet (wapili kulia), Msajili wa Hazina, Athman Mbuttuka (wakwanza kulia), Makamu Mwenyekiti wa Bodi Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (wakwanza kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.
**
Na Josephat Lazaro, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amepokea gawio la Sh. bilioni 17 linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dk. Ally Laay alimkabidhi Dk. Mpango hundi kifani ya fedha hizo jijini Dodoma leo Agosti 10,2020 mbele ya baadhi ya viongozi na mawaziri mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma yenye hisa ndani ya Benki ya CRDB na Menejementi yake.
Akizungumza katika hafla hiyo Dk. Mpango aliipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa gawio kwa serikalini na kupata matokeo mazuri ya fedha mwaka 2019 ambayo yamepelekea kuongezeka kwa gawio kwa Wanahisa ikiwamo Serikali.
“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa serikali kuwa benki hii inazidi kuimarika kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii,” alisema Dk. Mpango.
Dk. Mpango alisema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitakwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeianisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2020/2021.
“Kipekee kabisa niipongeze Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB kwa kazi nzuri mnayoifanya,” aliongezea Dk. Mpango.
Aliipongeza Benki ya CRDB kwa matokeo mazuri ya fedha iliyopata katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2020 ambapo faida ya Benki imeongezeka kwa asilimia 15 kufikia Sh. Bilioni 70.4 kutoka Sh. Bilioni 61.1 zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2019.
“Mkiendelea na kasi hii mwakani tunategemea kupata gawio nono zaidi,” alisema Dokta Mpango na kubainisha umuhimu wa ushiriki wa taasisi za fedha katika maendeleo ya taifa huku akiipongeza Benki ya CRDB kwa kupunguza riba ya mikopo ili kuchochea shughuli za maendeleo nchini.
Dk. Ally Laay alisema gawio hilo ni sehemu ya faida ya Sh. Bilioni 120.1 baada ya kodi ambayo Benki ya CRDB na kampuni zake tanzu imeipata katika mwaka wa fedha 2019.
“Katika Mkutano wa Wanahisa uliofanyika kidijitali Juni mwaka huu, Wanahisa wa Benki ya CRDB walipitisha kwa pamoja gawio la Sh. 17 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 112.5 hivyo kufanya gawio la mwaka huu kufikia Sh. Bilioni 44.4,” aliongezea Dk. Laay.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alimhakikishia Dk. Mpango kuwa benki hiyo kupitia kauli mbiu yake ya ‘Tupo Tayari’ itaendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha nchini huku akielezea kuwa benki hiyo sasa hivi imejikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya kidijitali ya kutolea huduma ikiwemo CRDB Wakala, SimBanking, SimAccount na Internet Banking ambayo humsaidia mteja kupata huduma kwa urahisi, unafuu na haraka.
Akipokea gawio kutokana na uwekezaji wa Halmashauri za Mbinga, Lindi, Shinyanga, Mufindi, Chunya na Rungwe, Waziri wa TAMISEMI, Suleiman Jaffo alizihimiza halmashauri nyengine nchini kuweka katika hisa ili kupanua wigi wa mapato katika halmashauri zao.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Vijana, Jenista Mhagama alipongeza mifuko ya jamii ya PSSSF, NSSF na ZSSF kwa uwekezaji ndani ya Benki ya CRDB huku akiwataka viongozi wa mifuko hiyo kutumia gawio lalilopata kuboresha utendaji kazi ili kunufaisha wanufaika wa mifuko hiyo.
Serikali ndio mwanahisa mkubwa ndani ya Benki ya CRDB kutokana na kuwa na umiliki wa asilimia 21 kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA kushirikiana na Serikali ya Denmark, huku taasisi na mashirika ya umma yakiwa na umiliki wa hisa za asilimia 17.1.
Social Plugin