Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAUNDA KIKOSI MAALUMU KUKABILIANA NA FISI TISHIO MJINI SHINYANGA

Picha ya fisi
Na Suleiman Abeid - Shinyanga
KUTOKANA na kukithiri kwa matukio ya Fisi kushambulia wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga hususan watoto wadogo, serikali imeunda kikosi maalumu kwa ajili ya kufuatilia na kuwasaka fisi hao ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakiwasumbua wakazi wa manispaa hiyo.

Kwa takribani miezi sita sasa, kumekuwepo na matukio ya Fisi kuonekana katika maeneo mbalimbali ya mji wa Shinyanga ambapo huwashambulia watu na kuwasababishia majeraha huku ikiripotiwa watoto wasiopungua wanne kufariki baada ya kushambuliwa na fisi hao.

Tukio la hivi karibuni lilitokea katika kitongoji cha Relini mtaa wa Nhelegani Manispaa ya Shinyanga, mtoto aliyetambulika kwa jina la Kulwa Machiya (06) alikufa baada ya kujeruhiwa vibaya na Fisi aliyewavamia na kumshambulia wakati wakitokea machungani pamoja na watoto wenzake.

Kutokana na hali hiyo, Halmashauri imelazimika kuunda kikosi maalumu ambacho kitaendesha operesheni ya kuwasaka Fisi hao ili kuwaua na kuepusha wananchi kuendelea kuishi wa wasiwasi wa kushambuliwa.

Kiongozi wa kikosi hicho, Ezra Manjerenga amesema, operesheni hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya Wataalamu wa Maliasili Kitengo cha Wanyamapori, Jeshi la Polisi, viongozi wa vijiji husika wakiwemo walinzi wa Jadi (Sungusungu).

Kwa mujibu wa maelezo ya kiongozi huyo, tayari operesheni hiyo imeanza leo saa 12 alfajiri kwa kufanya msako katika vichaka na mapori yote yaliyopo katika kijiji cha Nhelegani kwenye vitongoji vya Itogwanh’olo na Ibanza.

Hata hivyo kiongozi huyo ametoa wito kwa wakazi wote wa maeneo ambako Opresheni inafanyika kutoa ushirikiano wao kwa kuelekeza maeneo ambayo fisi hao wamekuwa wakionekana mara kwa mara ili kuweza kukabiliana nao.

Chanzo - TimesMajira Online

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com