Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia Kamati ya Maudhui imekifungia kipindi cha Jahazi kinachorushwa na Clouds FM kuanzia leo tarehe 14 Agosti 2020 kutokana na kosa la kurusha maudhui yenye kuchochea kujichua sehemu za siri na ngono.
Akizungumza na waandishi wa Habari Mwenyekiti wa Kamati hiyo Joseph Mapunda amesema vyombo vya habari vinapaswa kuzingatia weledi na sheria zilizowekwa kwa maslahi mapana ya ukuaji wa tasnia ya habari.
Katika hatua nyingine kamati hiyo imetoa onyo kali kwa baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo Kiss FM kwa kukiuka kanuni za utangazaji kwa kurusha habari bila kuzingatia mizania ya habari kupitia kipindi cha Amka na BBC wakati wakimhoji Makamu Mwenyekiti wa CHDEMA, Tundu Lissu kuhusu wanachama wa chama hicho kuzuiwa kumuaga Hayati Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.
Pia kituo cha Redio One kimepewa onyo kali kwa kukiuka kanuni ya utangazaji kupitia Kipindi Amka na BBC kwa kurusha matangazo bila kuzingatia mizani. Walimhoji Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiituhumu serikali kuwazuia wanachama wa CHADEMA kumuaga Rais Mkapa.
Redio One walijitetea kuwa wana mkataba na BBC, na Redio One wanatakiwa kupokea na kurusha vipindi vilivyoandaliwa na BBC kwa sababu BBC ipo nchini kisheria.
Kamati ya Maudhui ya TCRA imesema Radio One wana usimamizi mbovu wa vipindi cha nje na utetezi wao hauna mashiko kwa wao wanapaswa kuzingatia sheria kwa chochote wanachorusha, na mkataba wao na BBC una mapungufu.
Kamati imeshauri uongozi wa Redio One na vituo vingine vilivyokutwa na makosa kuimarisha usimamizi wa maudhui, kupitia upya mikataba yao na vyombo vya nje. Kituo hicho kimepewa onyo kali na kimewekwa chini ya uangalizi kwa miezi mitatu.
Vituo vingine vilivyopewa onyo kali ni pamoja na Abood FM kwa Kufanya uzembe wa kutangaza habari bila kuzingatia mizania, CG FM, huku Wasafi Media Online TV wakipigwa faini ya milioni tano kwa kosa la kuhamasisha ngono kupitia kipindi cha Women Matters.
Mamlaka ya Mawasiliano imetoa wito kwa vyombo vya habari kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka hiyo katika uendeashaji na usimamizi wa vyombo vya habari.
Social Plugin