Patrobas Katambi
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mgombea wa Nafasi Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini,Patrobas Katambi (CCM) amewasili mkoani Shinyanga ambapo kesho Jumamosi Agosti 22,2020 atachukua Fomu ya Kugombea Ubunge kwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini tayari kwa kuanza rasmi mchakato wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2020.
Akizungumza na Malunde 1 blog, Katibu wa Siasa na Uenezi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini,Said Bwanga amesema Katambi ambaye ameteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM taifa (NEC) kugombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini, atachukua Fomu kesho majira ya saa tatu asubuhi katika ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini.
“Mgombea Ubunge Patrobas Katambi tayari amewasili Jimboni na kesho anatarajia kuchukua fomu kwa msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini akisindikizwa na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi, Madiwani walioteuliwa kupeperusha Bendera ya CCM katika uchaguzi Mkuu 2020 na Watia nia kugombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini mwaka 2020”,amesema Bwanga.
Amesema mara baada ya kuchukua fomu, Katambi ataelekea katika Ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga Mjini kwa ajili ya kusalimiana na wanachama wa CCM na wananchi wa Jimbo la Shinyanga Mjini.