Na Dinna Maningo,Tarime
Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Michael Kembaki amerejesha fomu ofisi ya msimamizi wa uchaguzi huku akisindikizwa kwa shangwe na furaha hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kusimamisha shughuli zao kwa muda na kumsindikiza mgombea.
Kembaki alisindikizwa na watu mbalimbali akiwemo mgombea ubunge Jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara,Viongozi wa CCM, wanachama wakiwemo vijana wa Green Gard na baadhi ya wananchi.
Wagombea hao wakitokea ofisi ya CCM wilaya ya Tarime walipita na kuzunguka maeneo ya mjini,stendi kuu ya mabasi wakicheza nyimbo za wasanii mbalimbali kwa shangwe na mbembwe huku wimbo wa Zuchu ".......jua lileee litelemke mama....."ukionekana kuwakosha wengi na kuwalazimu baadhi ya wananchi kusitisha shughuli zao na kuungana na wenzao kumsindikiza Kembaki kurejesha fomu.
Furaha hizo na shangwe zikawagusa hadi wafanyakazi wa Benki ya NBC kuacha shughuli zao na kusimama nje wakipunga mikono,na basi zilizokuwa zikipita zikasimama huku ikisikika milio ya honi.
Wagombea hao wakafika ofisi ya msimamizi ambapo Kembaki alimkabidhi fomu msimamizi wa uchaguzi Elias Ntiruhungwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Tarime.
Wakiwa wanaondoka punde si punde wakakutana uso kwa uso na wapinzani wao wa Chama cha CHADEMA ambao nao mgombea wao jimbo la Tarime mjini Esther Matiko akirejesha fomu.
Kukutana kwa CCM na CHADEMA kukaibua utani wa kisiasa kila mmoja akionekana ni zaidi kuliko mwenzake na muda mfupi wagombea wa CCM na wafuasi wao wakaendelea na safari na wafuasi wa CHADEMA wakaelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi.
Vijana Green Guard wakiongoza zoezi la kumsindikiza Mgombea Michael Kembaki kurejesha fomu
Wafuasi wa mgombea Ubunge jimbo la Tarime mjini kupitia CCM Michael Kembaki wakimsindikiza wakati akirejesha fomu
Wanachama wa CCM na CHADEMA wakikutana uso kwa uso wakati wagombea wao wa ubunge wakirejesha fomu ofisi ya msimamizi wa uchaguzi jimbo la Tarime mjini
Mgombea ubunge Jimbo la Tarime vijijini akiwa ofisi ya CCM kumsindikiza mgombea ubunge Tarime mjini Michael Kembaki kurejesha fomu
Social Plugin