Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : KEMBAKI AZINDUA RASMI KAMPENI UBUNGE TARIME MJINI …AAHIDI MAKUBWA AKICHAGULIWA, MAKADA WATIA NENO



Mgombea ubunge Jimbo la Tarime mjini kupitia chama cha Mapinduzi CCM Michael Kembaki akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni zake.
**
Na Dinna Maningo - Tarime
Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime mjini kupitia Chama cha Mapinduzi(CCM) Michael Kembaki amezinduka Kampeni ya kugombea ubunge huku  akiahidi kufanya maendeleo makuwa ikiwemo upatikanaji wa huduma ya maji safi ,miundombinu ya barabara na ujenzi wa Soko kuu.

Katika uzinduzi huo walihudhuria Viongozi na wanachama wa CCM, Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara,kada maarufu wa CCM na mmiliki wa Mabasi,Peter Zakaria ,Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa mkoa wa Mara Christopher Gachuma,Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara Samwel Kiboye (Namba Tatu) na wananchi.

Kembaki alisema kuwa Tarime haina maji safi na salama  na kwamba hata chanzo cha maji mto Nyanduruma hakitoshekezi mahitaji na wakati wa kiangazi chanzo hicho hukauka.

"Nashukuru chama changu kuniamini na kuniteua,kura mlizonipa 2015 wakati nagombea Ubunge zilinipa imani nikaamua kurudi ,ndugu zangu muungwana ni yule anayeshukuru hata kwa kidogo,najua kuna wananchi waliniamini walinipigia kura",alisema Kembaki.

Aliongeza "Nakumbuka ahadi nilizozitoa niliona kero mbalimbali nikajinyima na baadhi nikazitatua hii kero ya maji imekuwa ni kilio, chanzo cha maji kipo Kenyamanyori lakini hata wananchi wa hapo hawapati maji na ni machafu ukifua nguo nyeupe ina badilika rangi naomba mnichague nitatue kero ya maji na soko kuu lililotelekezwa kwa muda mrefu bila kujengwa nitahakikisha linajengwa".

Akizungumzia ubovu wa miundombinu ya barabara Kembaki alisema kuwa wilaya ya Tarime ina rasilimali nyingi ambapo barabara za mjini zote zilitakiwa kuwa za lami na si za vumbi.

"Akina mama wanauza matunda kwenye vumbi huwa nikipita na kuwaona roho inauma, mkinichagua ntahakikisha naboresha mazingira rafiki ya biashara ,waendesha pikipiki wanapata tabu pikipiki zinawahi kuharibika kwa sababu ya ubovu wa barabara", alisema Kembaki.

"Nimezunguka kata 8 nimechangia maendeleo mwenzangu Esther Matiko wa CHADEMA wakati wa kugombea 2015 aliahidi kujenga ghorofa shule ya msingi Sabasaba ahadi ambayo mpaka leo hajaitekeleza ila mimi nilisema sina uwezo ntajenga darasa la kawaida nanyi ni mashahidi mnaona wanafunzi wanasoma niliyoyaahidi nimetekeleza kwa asilimia 80 ",alisema Kembaki.

Mke wa mgombea huyo Magreth Rhobi aliwaomba wananchi kumpa kura mmewe ili afanye maendeleo.

Katika uzinduzi huo  baadhi ya makada wa CCM waliokuwa wakitia nia kugombea ubunge kupitia chama hicho akiwemo Jackson Kangoye aliyekuwa mshindi namba moja ambaye hata hivyo jina lake halikurudi na badala yake vikao vya chama Taifa  vilimteua Michael Kembaki wamehudhuria uzinduzi huo wa Kampeni .

Kangoye aliwashukia watu wanaoeneza maneno kupitia mitandao ya kijamii kuwa yeye hamuungi mkono Kembaki na kusema habari hizo ni za uongo.

"Nimesikia maneno mengi kuwa mimi simuungi mkono Kembaki ni uongo mimi nitashiriki na Kembaki katika kampeni zake tumsaidie aweze kushinda,aligombea 2015 kura hazikutosha saizi kajipanga na ninaamini tutashinda na ikiwezekana aongoze miaka 10",alisema Kangoye.

Manchare Suguta ambaye ni ndugu wa mgombea ubunge jimbo la Tarime vijiini John Heche aliwaomba wananchi kumpigia kura Kembaki na Mwita Waitara anayegombea jimbo la vijijini.

"Hatuna muda wa kupoteza hapa ni kazi tu kwahiyo ndugu zanngu tumpe kembaki ni mtu wa kazi msidanganyike hapa ni kazi tu",alisema Susy Chambili.

Veronica Nyahende alisema "Wana Tarime tumepata nafasi tusiicheze tuwape kura CCM kwa maendeleo ya Tarime,akina mama tumechoka kubeba maji kichwani.

Wakili wa kujitegemea Onyango Otieno alisema"tuna matatizo mengi maji yetu ni shida UTI,Typhoid ni nyingi tunamtuma Kembaki atuletee maji,bararaba ni shida kama ya Kenyamanyorii".

"Mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Vijana wa mkoani, nafahamu mambo mengi ambayo jimbo la Tarime mjini imeyakosa,huwezi kupata maendeleo kwa chama kisicho na Ilani  niwaombeni kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa ndiyo kosa mpigieni Kembaki",alisema Ditu Manko.

Hezbon Mwera alisema "Tarime mjini tunataka sasa tumtume Kembaki atuletee maendeo tunachohitaji sisi ni maendeleo tunataka mipango na miradi inayoonekana.

Mgombea ubunge viti maalum Mara Amina Makilagi aliwaomba wananchi" naomba mpigie CCM nina uzoefu ndani ya bunge sisi wabunge wa ccm tukikutana tunajadiliana kwanza kwenye vikao tupeni Kembaki atakayekwenda kusemea maendeleo, katika bajeti iliyopita tumepata mradi wa maji na Tarime imo,jiulize tangu tumepitisha fedha mbona hazijaja tupeni Kembaki maji yaje".

Roselina mgombea viti maalumu kundi la walemavu alisema "nashukuru kwa kunichagua hadi ngazi ya Taifa sisi watu wenye ulemavu tunapata shida hatuna mtu wa kutusemea nilitembelea shule moja hakuna vifaaa, walemavu wanahangaika mazingira si salama huku mgombea ubunge viti maalumu kundi la vijana akiwaomba vijana kumchagua Kembaki.

Wazee wa mila kutoka koo 12 za jamii ya Wakurya nao hawakuwa nyuma kumnadi Kembaki na Waitara, Nchagwa Mtongori mzee wa mila kutoka koo ya Wanchari alisema kuwa ili wananchi wapate maendeleo ni vema wachague CCM kwakuwa wao ni watekelezaji.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa Charles Mniko aliwataka wazee wa mila kuungana pamoja kuiwezesha CCM kushinda.

Kada wa CCM ambaye pia ni mmiliki wa mabasi ya Zakaria yanayofanya safari zake Sirari-Mwanza Peter Zakaria alisema"nimejitahidi kuchangia maendeleo hospitali ilikuwa imeoza hatukutumia pesa za Serikali hata sh.100 najua nilipopata matatizo mlilia sana sasa naomba msiniangushe niko salama mpeni kura Kembaki"alisema Zakaria.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Tarime Daud Ngicho  alisema kuwa Rais Magufuli ametatua kero nyingi ikiwemo ya uanzishwaji wa masoko ya dhahabu ambayo yamewawezesha wafanyabiashara kuuza dhahabu huku akiwalalamikia waliokuwa wabunge wa Tarime kutoka CHADEMA kuingilia kesi zisizowahusu na kushindwa kushughulikia kero za watu wa Tarime  hili hali hawakuwa na kesi kwenye majimbo yao wanayotoka.

Mjumbe wa Halmashauri ya Taifa mkoa wa Mara Christopher Gachuma alisema uzinduzi ulikuwa wa kuwatambulisha wagombea nakwamba anaimani CCM itashinda kwa kishindo.

Mwenyekiti wa chama CCM mkoa wa Mara Samwel Kiboye (Namba tatu) alisema kuwa baadhi ya wanaCCM ni vigeugeu.

"Safari hii hatutawakubali wasaliti ndani ya chama,Kembaki Unapoenda kuomba kura mtangulize mungu ukimtanguliza shetani hakusogelei na mungu hasemi uongo mungu mambo yake yamenyooka safari hii lazima tukomboe majimbo.

"Tunataka kampeni ya Kiungwana sisi ndiyo tuna Serikali lakini tunaomba kampeni za heshima,tutangulize mungu mbele kwa kila jambo,tumeshavunja makundi ,mimi saizi Waitara namuunga hatuna utofauti lengo letu tunataka CCM ishinde tofauti zetu tumeziondoa,wanaccm msilizike tafuteni kura."alisema Keboye

Naye mgombea Ubunge jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara alisema "wagombea wote wa upinzani nawafahamu,kama tunataka kero zitatuliwe nakuomba pigia CCM ,kama mnataka tuachane na maji ya tope pigia Kembaki,mimi niiliona nijipendekeze ili nipate miradi nikaingia CCM ,Ukija spidi nitakutuliza ,ukija taratibu nitatulia vijana tumejipanga hii ngoma mtoto hatumwi sokoni",alisema Waitara.
Umati wa watu wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge jimbo la Tarime mjini kupitia CCM Michael Kembaki
Katibu wa CCM wilaya ya Tarime Hamis Mkaruka wakicheza na wana CCM wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge jimbo la Tarime mjini
Wafuasi wa mgombea ubunge jimbo la Tarime mjini Michael Kembaki wakishangilia wakati wa uzinduzi wa kampeni
Wafuasi wa mgombea ubunge jimbo la Tarime mjini Michael Kembaki wakishangilia wakati wa uzinduzi wa kampeni
Wafuasi wa mgombea ubunge jimbo la Tarime mjini Michael Kembaki wakishangilia wakati wa uzinduzi wa kampeni.
Makada wa CCM wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni .Kulia ni mgombea ubunge jimbo la Tarime mjini Michael Kembaki,wapili kulia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara Samwel Keboye,wa kwanza kushoto ni mmiliki wa mabasi Peter Zakaria,wa pili kushoto ni Mjumbe wa NEC Christopher Gachuma
Wananchi wakicheza ngoma ya Ritungu wakati wa uzinduzi wa kampeni.
Wasanii wakitumbuiza wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge Michael Kembaki


Wasanii wakitumbuiza wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge Michael Kembaki

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com