Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami (kulia).
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Serengeti kimetangaza kuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kupitia CHADEMA Mhe.Tundu Anthipas Lissu pamoja na Mgombea Mwenza,ndugu Salum Mwalimu watazindua rasmi Kampeni za CHADEMA Uchaguzi Mkuu 2020.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari leo Jumapili Agosti 30,2020 Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi amesema Uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu CHADEMA utafanyika siku ya Jumatano Septemba 2,2020 katika viwanja vya Joshoni Lubaga Mjini Shinyanga kuanzia saa nane mchana.
“Ndugu Watanzania, watu wa Kanda ya Serengeti inayojumuisha Mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu napenda kuwajulisha kuwa Mgombea Urais Mhe.Tundu Anthipas Lissu pamoja Mgombea Mwenza,ndugu Salum Mwalimu watafika kwenye mkoa wa Shinyanga Septemba 2,2020 kuja kufanya uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu katika Kanda ya Serengeti”,amesema Ntobi.
Kwa upande wake, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami amesema ufunguzi wa kampeni za CHADEMA kwa Kanda ya Serengeti utawakaribisha wananchi na wanachama wa CHADEMA kutoka kwenye mikoa mitatu inayounda Kanda ya Serengeti ambayo ni Shinyanga, Simiyu na Mara ambapo pia tutakuwa na mapokezi maalumu ya mgombea Urais ambaye atatua katika uwanja wa Ndege Kahama kisha kuelekea Shinyanga Mjini.
“Tunawaomba wananchi kutoka vyama vyote wahudhurie kwa wingi kuja kumsikiliza Mgombea wetu wa Urais ana nini cha kuwafanyia baada miaka 58 ya utawala wa CCM ambapo wananchi pia watatumia fursa hiyo kuwasikiliza wagombea kupitia CHADEMA”,amesema Mnyawami.
Katika hatua nyingine Mnyawami amesema CHADEMA imekata rufaa kwenye kata na majimbo ambako wagombea wake hawajateuliwa kugombea ubunge na udiwani.
Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu leo Jumapili Agosti 30,2020 katika Ofisi za CHADEMA Kanda ya Serengeti Mjini Shinyanga. Kushoto ni Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi.
Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu leo Jumapili Agosti 30,2020.
Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari leo Jumapili Agosti 30,2020 kuhusu Uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu CHADEMA Kanda ya Serengeti ambapo Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kupitia CHADEMA Mhe.Tundu Anthipas Lissu pamoja na Mgombea Mwenza,ndugu Salum Mwalimuza watakuwa katika Jimbo la Shinyanga Mjini siku ya Jumatano Septemba 2,2020 katika viwanja vya Joshoni Lubaga Mjini Shinyanga kuanzia saa nane mchana.
Social Plugin