Ngariba mstaafu akitoa elimu kwa kundi la Wakunga wa jadi, mangariba, wazee mashuhuri, viongozi wa dini na vitongoji kwenye mjadala wa tathmini ya mwenendo wa ukatili wa kijinsia na namna ya kutokomeza vitendo hivyo ulioandaliwa na shirika la ESTL chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society katika Kata ya Msisi, Singida DC.
Mjadala ukiendelea.
Mjadala ukiendelea.
Afisa Mradi Rosemary Mfui akizungumza na vijana kwenye moja ya mafunzo yanayotolewa na ESTL
Afisa Mthamini wa mradi huo kutoka shirika la ESTL, Philbert Swai akizungumza na wajumbe wa Kamati ya MTAKUWWA ngazi ya kijiji kwenye moja ya mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia na vitendo vya ukeketaji yanayotolewa na shirika hilo.
Na Godwin Myovela, Singida
SHIRIKA lisilo la kiserikali la ESTL (Empower Society Transform Lives) limewakutanisha vijana, mangariba, viongozi wa dini, serikali ya kijiji na watu mashuhuri ndani ya kijiji cha Nkwae, Kata ya Msisi mkoani hapa ili kujadili kwa pamoja, sambamba na kufanya tathmini ya hali halisi ya mwenendo wa matukio ya ukatili wa kijinsia.
Wakizungumza jana kupitia kampeni ya ‘Tokomeza Ukeketaji Singida,’ chini ya uratibu wa ESTL kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS), wengi walisema vitendo vya ukeketaji na matukio ya ukatili wa kijinsia bado ni tatizo na kwamba maovu hayo hufanyika kwa siri kubwa.
“Hapa kijijini vitendovya ukeketaji bado vinafanyika. Na kuna siri kubwa baina ya mhanga na ndugu wa karibu, na endapo mwana-ndugu anavujisha siri hiyo huchukiwa na familia au hata ukoo husika na wakati mwingine kutengwa kabisa,” alisema kijana mkazi wa kijiji hicho Ally Mohamed.
Kijana mwingine, Firdaus Selemani alisema suala la mimba na ndoa za umri mdogo vimekuwa ni vitu vya kawaida na hakuna hatua zozote za maksudi zinazochukuliwa hata baada ya kumbaini mtuhumiwa..ndugu wanalindana na kila kitu kinamalizika kimya-kimya.
Kwa upande wa Mangariba na viongozi wengine wa MTAKUWWA ngazi ya kijiji wao walisema ili kukomesha matukio hayo ya ukatili serikali inapaswa kutoa nafasi kwa wajumbe wa kamati za mtakuwwa sambamba na kuweka ajenda ya masuala ya ukatili wa kijinsia kwa kila mkutano na vikao vya kisheria ili kusambaza elimu na kuhamasisha jamii kuondokana na mila potofu.
“Bado kuna changamoto ya kutoshirikishwa kwenye vikao rasmi na mikutano ya kijiji inayofanyika kwa lengo la kupeleka ujumbe huu wa kupinga ukatili wa kijinsia na vitendo vya ukeketaji,” alisema mmoja wa Ngariba.
Mwingine Sarah Mgimba alisema mtoto wa kike anapopatwa na tatizo la unyanyasaji wa kijinsia wengi hukaa kimya kwa hofu, na kama jirani kabaini tatizo na kutoa taarifa nae huonekana ana kihere-here. Hivyo kuna haja serikali kuwatambua viongozi wa kamati za ulinzi wa Mwanamke na Mtoto na kuwapa ushirikiano.
Hata hivyo, baada ya majadiliano hayo vijana wengi walipata mwamko na kujikuta wakihamasika hatimaye walikubaliana kuja na kauli moja isemayo ‘mabadiliko yanaanza na mimi’ na kwa kauli moja wamekubaliana kwa kila mmoja kubadili tabia huku wakiahidi kuwa chachu kwa jamii inayowazunguka.
Aidha, katika hatua nyingine kundi hilo la vijana wa kata ya Msisi chini ya ESTL walipata fursa ya kutengeneza ‘Mpango Kazi’ utakaowaongoza katika kutekeleza majukumu yao dhidi ya vita ya matukio ya ukatili wa kijinsia na ukeketaji.
“Shabaha ya mpango kazi wetu ni kutusaidia kuanza kuibua matukio yote ya ukatili, kuhamasisha jamii itoe taarifa na kufanya ufuatiliaji na hatimaye kutoa taarifa kwa MTAKUWWA na kwenye mfumo wa Tehama uliobuniwa na ESTL ili kutoa matukio ya ukatili, “ alisema Mohamed.
Kwa upande wake, Afisa Mthamini wa Mradi huo kutoka ESTL, Philbert Swai wameamua kuratibu kusanyiko hilo la vijana siku moja baada ya maadhimisho ya siku ya vijana duniani yaliyofanyika Agosti 12 mwaka huu, ili kutoa fursa kwa vijana wa Msisi kuungana na vijana wenzao duniani kote katika kufanya tathmini ya mwenendo wa matukio ya ukatili na namna bora ya kukabiliana nayo.
“Tumeona ni vema vijana hawa tukawapa jukwaa la kujadili, kufanya tathmini na kupata mwelekeo wa pamoja wa namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na masuala ya ukeketaji kwa mtoto wa kike,” alisema Swai.
Afisa mradi wa ESTL, Rosemary Mfui alisema ni wakati sasa wa kuwa na kasi ya uwajibikaji wa pamoja kwa kila mwana-singida kutimiza wajibu wake, ili kutokomeza kabisa ukatili wa kijinsia na viteno vya ukeketaji.
Naye, Afisa Vijana kutoka ESTL, Edna Mtui alisema anaamini vijana wakiwezeshwa wanaweza, na ushahidi ni kwamba kupitia kikosi kazi kilichoundwa, vijana hao wameazimia kupita kwenye mashule, michezoni, zahanati, kwenye mitandao ya kijamii ‘watsapp’ vicoba na kwingineko, lengo likiwa ni kusambaza elimu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Na Afisa Mradi Msaidizi wa ESTL, Annamaria Mashaka alisema “mbali ya juhudi kubwa zinazofanywa katika kuelimisha jamii- lakini bado vitendo vya ukeketaji na ukatili kwa mtoto wa kike vinaendelea, na hii ni kutokana na Kamati zilizopo za MTAKUWWA ngazi ya kijiji kutokukutana wala kupeana mrejesho wa chochote kinachoendelea.
Social Plugin