Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KALEMANI AAGIZA MRADI WA KUSAMBAZA UMEME SINGIDA UKAMILIKE IFIKAPO SEPTEMBA 10


Na Ismaily Luhamba Singida.
WAZIRI wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ametoa agizo kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini REA awamu ya pili Mkoa wa Singida pamoja na Shirika la umeme Tanzania TANESCO Mkoa huo kuhakikisha wanamaliza mradi huo ifikapo Septemba 10 mwaka huu.
Ametoa Agizo hilo jana wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi baada ya kutembelea Kijiji cha Kisiriri kilichopo Wilayani Iramba Mkoni Singida ambapo alikagua na kujionea kazi ya kusambaza umeme wa REA awamu ya pili ambapo inafanyika kwa kusuasua.
Dkt Kalemani aliitaka Kampuni ya JV MEMEC &DESCO ya Kitanzania inayotekeleza Mradi huo kuwa ifikapo Septemba 10 mwaka huu wawe wamekamilisha mradi huo.
“Nasema hivi kuanzia leo hakuna mtu kurudi mjini hasa nyinyi wakandarasi, mtabaki huku mpaka tarehe 10 nitakapo kuja mimi mwenyewe kwenye uzinduzi na uwashwaji umeme katika Vijiji vyote 51 ili kumaliza huu mgogoro, nawataka hawa wakandarasi Tanesco pamoja na Rea wawe wanakwenda kusaini kila siku katika kituo cha Polisi kilichopo karibu na sehemu wanayo fanyia kazi na mimi niwe napatiwa taarifa kila wiki”, alisema Kalemani.

Pia Kalemani aliwataka Tanesco kuipima Kampuni ya JV EMEC & DESCO kwa siku saba kama kweli wanaweza kumaliza kazi hiyo kwa muda aliyowapa, na kama hawawezi kumaliza kwa wakati wavunje huo mkataba na kampuni hiyo.
Aidha ameipongeza kampuni ya CCCE ETERN CONSORTIUM LTD ya Kichina ambayo inatekeleza mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza kwa kufanikiwa kusambaza umeme kwenye Vijiji 1680, ambapo vimebaki  vijiji 26 kwa Mkoa mzima ili kumaliza kazi ya kusambaza umeme.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo, Dkt Rehema Nchimbi amesema atahakikisha anasimamia maelekezo hayo ili kabla ya muda uliopangwa na Waziri kuisha mradi huo uwe umekamilika.
“Kupitia kamati yangu ya ulinzi na usalama nitahakikisha mkandarasi anakwenda kituo cha polisi kila siku na kusaini kama ulivyoagiza na ripoti hiyo nitakutumia mimi mwenyewe”, alisema Dkt Nchimbi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com