Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (kushoto) akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, viongozi wa Kata ya Mwaru pamoja na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, wakati akikagua Msitu wa Minyughe ambao umevamiwa na kufanyika uharibifu mkubwa wa mazingira.
Miti ikiwa imekatwa kwenye msitu huo.
Miti ikiwa imekatwa kwenye msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (katikati) na wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa Kata ya Mwaru wakiangalia mkaa uliotelekezwa na wavamizi katika msitu huo.Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (katikati) akiwaonesha wajumbe wa kamati hiyo mkaa uliotaifishwa na Serikali baada ya kutelekezwa na wavamizi katika Msitu wa Minyughe wilayani humo mwishoni mwa wiki wakati akikagua msitu huo. Kulia ni Mshauri wa Jeshi la Akiba wa wilaya hiyo, Capteni Gabriel Chabimia na Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Ikungi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Stephano Chaula.
Miti ikiwa imekatwa kwenye msitu huo.
Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Mwaru, Mohamed Mrisho (katikati) akielezea uharibifu wa msitu huo.
Ulinzi ukiimarishwa wakati wa ukaguzi wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (kushoto) akizungumza na mtoto Soud Seme anayeishi na wazazi wake ndani ya msitu huo.
Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Mwaru,wakimwaga mkaa uliohifadhiwa kwenye viroba na wavamizi wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (kushoto) na wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa Kata ya Mwaru wakiangalia mkaa uliotelekezwa na wavamizi katika msitu huo.
Mhifadhi Misitu Wilaya ya Ikungi (DFC), Wilson Pikoloti akizungumzia uharibifu wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwaru, Mwinyimvua Midelo , akizungumzia uharibifu wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha wa Kijiji cha Mwaru, Shabani Nyombe akizungumzia uharibifu wa msitu huo.
Mjumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii wa Kijiji cha Mwaru, Johari Haji, akielezea uharibifu wa msitu huo.
Safari ya ukaguzi wa msitu huo ikiendelea.
Na Dotto Mwaibale, Singida.
HALI ya Msitu wa Minyughe uliopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imeendelea kuwa mbaya kutokana na wakazi wanaouzunguka kuuvamia kwa kukata miti hovyo na kuingiza mifugo bila ya kufuata taratibu.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo mwishoni mwa wiki ilitembelea na kujionea hali halisi na namna uvunaji wa mazao ya msitu huo ikiwemo ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa ukifanyika bila ya kufuata utaratibu wimbi kubwa la wahamiaji kutoka mikoa ya jirani wakihusishwa na uharibifu huo.
Msitu huo wenye ukubwa wa takribani hekta 230,000 upo katika Tarafa za Sepuka, Ihanja na Ikungi na kuundwa na vijiji 26 wilayani Ikungi.
Msitu huo ulianzishwa chini ya mradi wa LAMP (Land Management Programme) ukifadhiliwa na Shirika la Sida la Uswisi mwaka 2002.
Msitu huo una uoto wa asili wa miti jamii ya miombo na maeneo kidogo ya mbuga na uoto adimu wa vichaka vya Itigi (Itigi Thickets) huku ukiwa na wanyamapori na viumbe wengine wa aina mbalimbali ambao walifanya makazi ndani ya msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya, Edward Mpogolo akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, viongozi wa Kata ya Mwaru pamoja na waandishi wa habari wakati akikagua msitu huo alisema lengo la kuuanzisha ilikuwa ni kutunza uoto wa asili na bioanuwai zilizokuwa hatarini kutoweka ikiwemo wanyamapori
Alitaja lengo lingine kuwa ni kutunza mazingira kwa ujumla na kupambana na hali ya kuenea kwa jangwa, kutunza rasilimali asili kwa kizazi kilichopo na kijacho pamoja na jamii kunufaika moja kwa moja na rasilimali misitu zilizopo.
Mpogolo alisema msitu huo ni nguzo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi ukiungana na msitu wa mikoa ya Tabora, Rukwa na Katavi katika kuimarisha mvua zitokazo misitu ya Kongo.
"Msitu huu ni chanzo cha maji ya Ruaha Mkuu ( Internal Drainage) ukiunga pori la akiba la Rungwa, Muhesi na Kizigo lililopo Manyoni", alisema Mpogolo.
Alisema msitu huo ni kidaka maji ( Catchment Forest) kwa bonde la Wembere linaloweka uhai wa Ziwa Kitangiri na Eyasi.
Mpogolo alitoa maagizo ya kuwachukulia hatua watu wote waliovamia msitu huo kwa kujenga na kuingiza mifugo yao ambapo alitaka orodha yao ikiwa na kuondoka mara moja ndani ya msitu ndipo wafanye utaratibu wa kuomba upya kwa serikali ya kijiji.
"Haiwezekani kuingia kwenye hifadhi bila ya kufuata taratibu na kufanya uharibifu huu mkubwa, Serikali ya kijiji na kamati yangu ya ulinzi na usalama ni lazima tuhakikishe uhalibifu huu wa msitu haujirudii tena", alisema Mpogolo.
Alisema hali hiyo ikiachwa eneo hilo litakuwa jangwa na jamii inayoishi humo itapata matatizo ya maisha kwani hata madawa yatokanayo na miti ya asili hayata patikana.
Mpogolo alitumia nafasi hiyo kuwaagiza viongozi wa halmashauri ya kijiji katika eneo hilo kuitisha mkutano utakaowakutanisha wavamizi hao na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo ili kujua walipateje kibali cha kuingia kwenye hifadhi hiyo kwani yamekuwepo madai ya watu kuwa kuna baadhi ya viongozi wasio waaminifu wa vijiji vinavyozunguka msitu huo kuchukua fedha au ng'ombe kutoka kwa wafugaji hao na kuwagawia ardhi katika hifadhi.
Alisema kupitia mkutano huo watawabaini viongozi waliojihusisha kwa namna moja au nyingine kutoa maeneo kwenye hifadhi hiyo nao watachukuliwa hatua za kisheria huku wavamizi hao wakifanyiwa utaratibu na halmashauri wa kutafutiwa maeneo mengine ya kuishi na kufanya shughuli za kilimo na ufugaji nje ya hifadhi.
Aidha Mpogolo alisema mvamizi atakaye kahidi hatua hizo za awali za mazungumzo na kuwasikiliza atachukuliwa hatua kali ikiwemo kuondolewa kwa nguvu ndani ya hifadhi hiyo.
Social Plugin