Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi (kushoto) akimkabidhi fomu mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Miraji Mtaturu wilayani humo jana.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi (kushoto) akimkabidhi fomu Mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Magharibi, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Elibariki Kingu wilayani humo jana.
Msafara wa boda boda ukimsindikiza Mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Miraji Mtaturu kwenda kuchukua fomu.
Shamra shamra za Wana CCM wakati wa kumsindikiza Mtaturu kwenda kuchukua fomu.
Miraji Mtaturu akionesha fomu hiyo baada ya kukabidhiwa.
Miraji Mtaturu akizungumza na Wana CCM waliomsindikiza kwenda kuchukua fomu.
Miraji Mtaturu (wa pili kushoto) akiserebuka na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Ikungi baada ya kuchukua fomu. Wa tatu kulia mwenye kofia ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo na kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Mika Likapakapa.
Mtaturu akiwashukuru wananchi (hawapo pichani) waliomsindikiza kuchukua fomu. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo na kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Mika Likapakapa. .
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu akiwa katika picha ya pamoja na Wana CCM baada ya kukabidhiwa fomu.
Kingu akizungumza na Wana CCM na kuwashukuru baada ya kuchukua fomu.
Dotto Mwaibale na Ismail Luhamba, Singida.
WAGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki (CCM) Miraji Mtaturu na Elibariki Kingu wa Singida Magharibi, wamechukua fomu za kuwania ubunge kwa mara nyingine tena baada ya kupitishwa na chama chao cha Mapinduzi (CCM) na kutakiwa kufanya kampeni za amani na kistaarabu.
Akiwakabidhi fomu hizo jana kwa nyakati tofauti Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Ikungi yenye majimbo mawili ya Singida Mashariki na Magharibi, Justice Kijazi aliwaambia mara kampeni zitakapoanza wahakikishe zinakuwa za amani na wala sio za vurugu.
"Kwa niaba ya Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) sisi tupo na tunawakaribisha na yapo masharti mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi huu moja ya mambo ambayo mtapewa ni kanuni za maelekezo lakini pia tunaomba uchaguzi wetu uwe huru na haki ambao hauna vurugu kama vile tunavyosema.
Tanzania yetu hii hatuna nchi nyingine ambayo tutaweza kwenda kufanya kazi wala hakuna nchi nyingine ambayo tukiharibu amani hii tuliyonayo tutaweza kwenda kukimbilia hivyo nawahasa vyama vya siasa na wagombea wote kuzingatia hayo kwani kesho kutwa tunaingia kwenye zoezi la kampeni hivyo twende tukafanye kampeni za kistarabu tuuze sera zetu kwenye vyama alafu baada ya tarehe 28 mwezi wa 10 kila mtu atachagua na kuona anamtaka nani.
Ninachoshukuru ni kwamba kila mgombea aliyechukua fomu amenihakikishia kuwa wataenda kufanya kampeni za amani na kueleza sera zao na wananchi watamchagua kiongozi wanaye mtaka." alisema Kijazi.
Kijazi alisema mpaka jana katika jimbo la Singida Mashariki wagombea waliokwisha kuchukua fomu walikuwa ni 13 na kwa upande wa Jimbo la Singida Magharibi walikuwa sita.
Wagombea hao wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kuchukua fomu walimhakikishia msimamizi huyo wa uchaguzi kuwa wataenda kunadi sera za chama chao cha CCM na si kuleta vurugu na kuhakikisha kinapata ushindi mnono kuanzia kura za ubunge, udiwani na Rais.