Na Bakari Khalid
Waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya habari vya kijamii wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuzingatia maadili ya uandishi wa habari ikiwamo kuandika habari za ukweli na uhakika ili kuepusha upotoshaji na kujiingiza katika migogoro hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi mkuu nchini.
Hayo yamesemwa jana Jumanne August 11,2020 na Kaimu mwenyekiti wa mtandao wa vyombo vya habari vya kijamii nchini-TADIO Bw:Anthony Masai wakati akifungua warsha ya siku sita (6) yenye lengo la kuongeza uhamasishaji juu ya Maadili ya Vyombo vya Habari na Kuripoti juu ya Hali ya Migogoro na Mabadiliko ,warsha inayofanyika katika Hoteli ya Kings Way mjini Morogoro.
Bwana Masai amesema mafunzo haya yana umuhimu mkubwa na TADIO inabeba jukumu lake la kuwakumbusha juu ya maadili ya uandishi wa habari lakini utekelezaji unabaki kwa mwandishi mwenyewe ,hivyo ni vyema kufuata maadili ili kuzuia migogoro isiyo ya lazima.
“kila mwandishi wa habari analo jukumu la kuhakikisha anafuata maadili ya uandshi wa habari kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kuzuia kuingia kwenye migogoro”,alisema Masai.
Kwa upande wake Mwandishi wa habari na Mtangazaji Mkongwe na Mwezeshaji wa Mafunzo hayo Bi.Rose Haji Mwalim;amesema kila muandishi ana wajibu wa kujitathmini juu ya kile anachokifanya kwani kwa kufanya hivyo itakusaidia kufanya kazi zao kwa uhuru zaidi.
Bi.Rose ameongeza kuwa waandishi wa habari hasa wa zama hizi baadhi yao yamekuwa wakikengeuka katika uandishi wao hivyo ni vyema kufuata maadili ya taaluma ili kuepusha migogoro.
Mafunzo haya siku sita (6) yaliyoandaliwa na mtandao wa vyombo vya habari vya kijamii nchini-TADIO kwa ufadhili wa shirika la kimatatifa linaloshughulika na elimu ,sayansi na utamaduni –UNESCO yamekutanisha mameneja wa vituo vya redio za kijamii 35 waliomo kwenye mtandao huo.
Social Plugin