Picha : WAANDISHI WA HABARI SHINYANGA WAPIGWA MSASA UANDISHI HABARI ZA MAGONJWA YA MLIPUKO


Daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Godfrey Mboye akitoa mafunzo ya magonjwa ya mlipuko kwa waandishi wa habari wanachama wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) leo Agosti 11, 2020 mjini Shinyanga


Na Damian Masyenene –Shinyanga Press Club Blog 
KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) kwa kushirikiana na Umoja wa Klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) imeendesha mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari ambao ni wanachama wa klabu hiyo juu ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo COVID-19 na namna ya kujilinda, kufanya kazi na kujikinga kwenye magonjwa hayo. 

Mafunzo hayo yamefanyika leo Agosti 11, 2020 katika ukumbi wa Vijana Centre Ngokolo mjini Shinyanga, yakiwezeshwa na wataalamu wa afya kutoka ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino. 

Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Richard Mhangwa amewashukuru wanahabari kwa mchango wao mkubwa katika kuwafikia wanajamii kwa utoaji wa huduma za afya. 

“Mafunzo haya ni mkono utakaotusaidia kuifikia jamii kutokana na umuhimu wa tasnia hii katika kuifikia jamii na tumeendelea kushirikiana kufikisha ujumbe mbalimbali kwenye jamii….tumetoa mafunzo kuhusu magonjwa ya mlipuko kwa sababu yanagusa sehemu kubwa ya jamii na njia zake za uenezaji ni rahisi kuzuilika kupitia elimu,” amesema. 


Katibu Mtendaji wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga, Ali Lityawi amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wanahabari kuelimisha, kuonya na kushauri jamii na pia kuwasaidia kuongeza ujuzi kwa kuelewa kwa upana namna ya kujikinga na kuchukua taarifa kuzipeleka kwa jamii bila kudhurika. 

“Ni mpango mkakati wa UTPC kwa kushirikiana na klabu za waandishi wa habari kwa kutoa mafunzo mbalimbali, Wanahabari ni kioo hivyo ni jukumu lao kuwa wa kwanza kupata elimu kwa kujielimisha wao binafsi, kuzikinga familia na wanajamii na kutoa taarifa sahihi lakini pia kushirikiana na serikali,” amesema.

Mtaalam wa Usalama wa Afya ya Kimataifa, Onesmo Mwegoha, mbaye pia ni Daktari wa binadamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, amesema zaidi ya asilimia 70 ya magonjwa yanayosababisha mlipuko yanatoka kwa wanyama kuja kwa binadamu, pia wakati wa magonjwa hayo huzuka nadharia na taarifa nyingi za uzushi ambazo zinapaswa kudhibitiwa. 

Mwegoha amesisitiza kuwa endapo jamii zetu zitazingatia usafi, basi magonjwa mengi ya mlipuko yatakuwa yamemalizwa. 

Kwa upande wake Daktari Godfrey Mboye kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, amesema lengo kubwa la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari jinsi ya kujikinga na kuongeza uelewa, huku akihimiza wananchi kuzingatia ulaji wa vyakula vyenye kuimarisha kinga ya mwili (hususan vyakula vya wanga/protini) ili kupambana na maambukizi ya COVID 19. 

Kwa upande wake, Mwandishi wa habari na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Alex Mchomvu, amesema wanahabari wanapaswa kupeleka taarifa zilizo sahihi kwa wakati muafaka kupitia vyombo sahihi ili jamii iwe salama. 

“Tuna kazi kubwa kama wanajamii kufanya kazi ambayo jamii inataka, kwenye dharura ama majanga, taarifa sahihi na vyombo vya habari vinaweza kusaidia kuokoa maisha, kuongeza kujiamini na kuchukua hatua (kuimarisha nguvu ya uokoaji). 

“Pia kuwawezesha watu kujisaidia, kuweka matumaini, kuongeza ushirikiano wa umma na kuzuia uzushi na taarifa za uongo,” amesema. 

Akifunga mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa shinyanga (SPC), Greyson Kakuru amewataka waachama wa chama hicho kudumisha umoja, kulipa ada kwa wakati ili kuendelea kunufaika na mafunzo hayo, huku akiwahimiza walionufaika na mafunzo hayo kuwajibika kwa vitendo kwa kuandaa habari zitakazohusu magonjwa ya mlipuko na kuchukua tahadhari wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kwa kuandaa taarifa sahihi na kujiepusha na habari za upande mmoja. 

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Richard Mhangwa akizungumza katika mafunzo ya magonjwa ya mlipuko kwa waandishi wa habari wanachama wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga (SPC)

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Greyson Kakuru akizungumza katika  mafunzo ya magonjwa ya mlipuko kwa waandishi wa habari wanachama wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga (SPC)
Katibu Mtendaji wa SPC, Ali Lityawi (katikati) akizungumza wakati wa  mafunzo ya magonjwa ya mlipuko kwa waandishi wa habari wanachama wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga (SPC)
 Mtaalam wa usalama na afya ya kimataifa, Dk. Onesmo Mwegoha ambaye pia ni Daktari wa binadamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mkoa huo
 Mafunzo yakiendelea kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga
 Waandishi wakiendelea kuweka umakini wakati wa uwasilishaji wa mada kwenye mafunzo hayo
  Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari mkoa wa Shinyanga wakifuatilia mafunzo
 Waandishi wakiendelea kufuatilia uwasilishaji wa mada mbalimbali wakati wa mafunzo hayo
 Waandishi wakiendelea kuandika vitu muhimu wakati wa uwasilishaji mada mbalimbali kwenye mafunzo hayo
 Mwenyekiti wa SPC, Greyson Kakuru (Kulia) na waandishi wenzake wakifuatilia mafunzo

 Waandishi wa habari wakifuatilia mafunzo hayo kwa umakini mkubwa

Mafunzo yakiendelea

 Mwandishi wa Habari wa Kituo cha ITV/Redio One mkoani Shinyanga, Frank Mshana akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo

 Dk. Onesmo Mwegoha akiendelea na mafunzo
 Mwandishi wa habari wa kituo cha Faraja Fm, Simeo Makoba (kulia) akichangia hoja
 Waandishi wa habari wakifuatilia kwa umakini mafunzo hayo
 Waandishi wa habari wakijadiliana kwenye makundi kuhusiana na mada mbalimbali zilizowasilishwa
 Majadiliano yakiendelea
  Waandishi wakijadiliana katika makundi
 Mhadhiri wa masuala ya habari kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Mwanza, Alex Mchomvu akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga
 Mtangazaji wa kituo cha redio cha Faraja FM, Isaac Edward (Isack wa Edo) akifafanua hoja mbele ya wenzake
 Waandishi wa habari wakiendelea kufuatilia hoja mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa
 Mwandishi wa habari wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd inayozalisha magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Rai na Dimba, Damian Masyenene akifafanua hoja wakati wa mafunzo hayo
 PICHA NA SHINYANGA PRESS CLUB



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post