Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Bilioni 3 Zatolewa Kuongeza Uzalishaji Mbegu Bora Za Mkonge- Kusaya

Serikali imefanikiwa kutoa shilingi Bilioni Tatu katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kuongeza utafiti na uzalishaji wa mbegu bora za mkonge zitakazo gawiwa kwa wakulima kwenye mikoa 17 inayolima zao la mkonge nchini.
 
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ametoa kauli leo  akiwa ziarani Mkoa wa Tanga kufanya ufuatiliaji wa maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa mwezi Juni mwaka huu.
 
”Serikali ya Awamu ya Tano tayari imekipatia kituo cha Utafiti TARI Mlingano Bilioni 3 za kukiwezesha kuongeza utafiti na uzalishaji mbegu bora zenye kutoa mavuno mengi ambazo zitagawiwa kwa wakulima wa mkonge nchini” amesema Kusaya

Kusaya alisema lengo la Wizara ya Kilimo ni kuona kituo cha Utafiti TARI Mlingano kinazalisha mbegu bora Milioni Tano mwaka huu 2020/21 ili zigawiwe kwa wakulima waongeze uzalishaji wa mkonge toka tani 36,000 za sasa kufikia lengo la tani 120,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

Ili kufikia lengo hilo la uzalishaji mbegu bora za mkonge Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti TARI Mlingano Dkt.Beatrice Senkoro alimweleza Katibu Mkuu kuwa wameanza kutekeleza kwa kuongeza eneo linalolimwa mbegu toka hekta 2 za sasa hadi hekta 65 .

”Jumla ya hekta 65 zimelimwa ambapo kati yake hekta 15 zimepandwa miche ya mkonge ipatayo milioni moja na laki Tano kufikia mwezi huu Agosti mwaka huu”
alisema Dkt.Senkoro.

Dkt.Senkoro ameiomba Wizara kuendelea kukiwezesha kituo hicho kuwa na maabara ya kisasa ili kiweze kuongeza kasi ya Utafiti wa mbegu bora za mkonge kwa njia ya " Tissue Culture Laboratory" inayotoa matokeo mazuri na mbegu nyingi.
 
Aliongeza kusema mahitaji ya mbegu bora za mkonge kwa wakulima wadogo nchini kwenye mikoa yote 17 inayolima yamefikia Milioni Moja na Laki Mbili wakati lengo la Wizara ni kuzalisha mbegu bora Milioni Tano kwa mwaka.
 
Dkt.Senkoro alitaja pia mafanikio ya Kituo cha TARI Mlingano ni pamoja na kuwafundisha kanuni bora za kilimo cha mkonge kwa Maafisa Ugani 427 na pia kimetoa mafunzo kwa wakulima 22,000 wakati wa Maonesho ya Kilimo Nanenane mkoani Simiyu ikishirikiana na Bodi ya Mkonge Tanzania.
 
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Kusaya ameitaka Menejimenti ya Bodi ya Mkonge ( TSB) kufanya sensa ya wakulima wa mkonge na kiasi cha eneo wanalolima ili mashamba yasiyolimwa Wizara ishauri serikali kuyatwaa na kuwapa wawekezaji wenye uwezo.

Kusaya ameelekeza pia Bodi hiyo ya Mkonge kusimamia zoezi malipo ya wakulima wa majani ya mkonge wanaodai kutolipwa na AMCOS na pia kudhibiti vitendo vya baadhi ya wakulima kuvuna mkonge usiokomaa na kuharibu ubora unatotakiwa .

Katibu Mkuu katika ziara hiyo ameipongeza Bodi ya Mkonge kwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu la kuhamia kwenye jengo lao la Mkonge House jijini Tanga.

” Nimefurahi leo kuona Bodi imehamia kwenye jengo hili la Mkonge House kama alivyoagiza Waziri Mkuu,sasa nataka mfanye kazi kubwa kusimamia uongezaji uzalishaji wa mkonge kwa wakulima zaidi kuhamasishwa kulima ili ardhi yote iliyokusudiwa kupandwa mkonge ilimwe”alisisitiza Kusaya

Katika hatua nyingine Kusaya alisema tayari serikali imetoa shilingi Milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la Ofisi ya Bodi hiyo ili liwe bora baada ya kutwaliwa kutoka kwa mwananchi aliyemilikishwa kinyume na utaratibu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania Saad Kambona alisema tayari kazi ya usajili wa wakulima wa mkonge imeanza na kuwa wakulima 7,551 wadogo wa mkonge wamesajiliwa kwenye mkoa Tanga ,Kilimanjaro na Morogoro.
 
Kambona amesema Bodi yake itaendelea kuhamasisha na kuelimisha wakulima wengi kuanzisha mashamba mapya ya mkonge na kupanda mbegu bora ili uzalishaji uweze kukua zaidi.
 
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo huyo ametembelea pia kiwanda cha kuzalisha mbolea cha ABM Tanga kukagua uzalishaji wa mbolea.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com