Mwigizaji nyota wa Marekani Chadwick Boseman enzi za uhai wake
Boseman hakuwahi kusema hadharani kuhusu maradhi yake
Mwigizaji nyota wa Marekani Chadwick Boseman, aliyefahamika sana kwa filamu ya Black Panther amefariki dunia kwa ugonjwa saratani akiwa na umri wa miaka 43.
Boseman amekufa nyumbani huko Los Angeles akiwa na mke wake na familia, kulingana na taarifa iliyotolewa kwenye mitandao ya kijamii.
Boseman alipatikana na saratani ya utumbo mpana miaka minne iliyopita lakini hakuwahi kusema hilo hadharani.
Taarifa za kifo chake zimeacha mashabiki wake kote ulimwenguni na mshutuko mkubwa.
Mwongozaji wa filamu ya 'Get Out' Jordan Peele, amesema kwamba hilo "ni pigo kubwa".
"Mpiganaji haswa, Chadwick alivumilia yote na kuwaletea filamu nyingi tu ambazo mumetokea kuzipenda," familia yake imesema kwenye taarifa.
"Kuanzia filamu ya Marshall to Da 5 Bloods, Ma Rainey's Black Bottom ilioandikwa na August Wilson na nyingine nyingi - filamu zote hizo zilitengenezwa wakati anapitia upasuaji na kupokea matibabu ya kemikali yaani kemotherapi. Ilikuwa fahari katika taaluma yake kushiriki kwenye filamu ya Black Panther."
Boseman alikuwa maarufu katika filamu ya michezo ya '42' ya mwaka 2013 kuhusu ubaguzi aliofanyiwa mchezaji wa kulipwa wa besiboli Jackie Robinson na ile ya 'Get on Up' mwaka 2014 kuhusu maisha ya mwimbaji wa nyimbo aina ya soul James Brown.
Hata hivyo, kama mhusika wa filamu ya Black Panther ndio atakayokumbukwa nayo zaidi.
Nyota huyo, Boseman, aliigiza kama mtawala wa Wakanda, filamu iliyoangazia Afrika ya kufikirika yenye teknolojia zilizoendelea sana za kisasa.
Pamoja na sifa alizopokea na kupata zaidi ya dola bilioni 1.3 za Marekani kupitia sinema kote ulimwengini, filamu hiyo ilichukuliwa sana kama hatua iliyopigwa kitamaduni kwa misingi ya filamu inayofanya vizuri mno ambayo waigizaji na mwelekezi, Ryan Coogler, wote ni watu weusi.
Mwaka jana, Boseman alisema filamu hiyo imebadilisha mtazamo wa kuwa "kijana, mwenye kipaji na mweusi".
Uzinduzi wa Filamu ya Black Panther, Kisumu Kenya
Black Panther ilikuwa filamu ya kwanza yenye maudhui ya ushujaa kuchaguliwa kama yenye picha bora katika tuzo la Oscar.
Pia aliigiza kama mhusika wa aina hiyo hiyo katika filamu nyingine nyingi mfano: Civil War, Avengers: Infinity War na Avengers: Endgame.
Filamu ya 'A sequel' ilikuwa inaendelea kufanyiwa kazi na ilitarajiwa kutoka mwaka 2022 huku Boseman akitarajiwa kurejea tena.
Taarifa za kifo chake zimeshutua wengi wakati ambapo hajawahi kuzungumzia ugonjwa wake hadharani.
Hata hivyo mashabiki walikuwa na wasiwasi kuhusu afya yake mwaka mmoja uliopita kwasababu ya kupunguza uzito kupita kiasi.
Tayari watu wameanza kutuma risala za rambirambi akiwemo mwigizaji na nyota mwenzake katika filamu ya Marvel Mark Ruffalo.
Mwigizaji Dwayne Johnson ameandika kwenye mtandao wa Twitter: "Asante kwa kungara kwenye na tasnia yako na kushirikisha dunia kipaji chako. Upendo wangu na maombi ni kwa familia yako."
Wanasiasa pia wameanza kutuma risala zao ikiwemo aliyeteuliwa kuwa makamu rais wa mgombea urais wa chama cha Democratic Kamala Harris.
Mwaka 2018, Boseman alirejea kwenye chuo kikuu alichosomea na kuzungumza katika sherehe ya kuhitimu kwa mahafali.
"Wengi wenu hapa wanapitia wakati mgumu dhidi ya chuo chenyewe," alisema hivyo katika hadhara ambayo wengi wao walikuwa ni kutoka kundi la walio wachache.
"Wengi mutamaliza Howard na kujiunga na mifumo na taasisi ambazo zina historia ya ubaguzi wa rangi na kutengwa.
"Lakini ukweli wa kwamba mumepambana katika chuo hiki ambacho munakipenda ni ishara tosha kuwa munaweza kutumia elimu yenu kuboresha dunia mutakayojiunga nayo."
CHANZO BBC SWAHILI
Social Plugin