Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC BARIADI AWATETEA WAKULIMA WA ZAO LA PAMBA

Samirah Yusuph

MKUU wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Festo Kiswaga, ameongoza  mnada wa zao la pamba katika kata ya Nkololo ili kuhakikisha kuwa anaongeza ushindani wa manunuzi katika zao hilo.


Pamba hiyo imeuzwa katika makampuni matatu ambayo ni Alliance Ginnery, Olam na Birchand ambazo zimenunua kwa bei ya shilingi 900.

Kiswaga aliyasema hayo jana mara baada ya kufanya mnada wa pamba katika kitongoji cha Isanga, kijiji na kata ya Nkololo na kuwataka wanunuzi wa pamba kununua pamba kwa kushindana kwa bei ya kuanzia shilingi 900 pia wakulima walipwe fedha taslimu.

"Sitaki kuona mkulima wa pamba anakopwa fedha yake bali wakulima walipwe fedha taslimu ili kuondokana na matapeli wa pamba wanaopunja wakulima kwa kutoa bei ndogo ya shilingi 800, 850 hadi 700 kwa kilo moja," alisema Kiswaga.

Kutokana na mahitaji ya pamba kuongezeka Kiswaga amemuagiza afisa Ushirika wa wilaya hiyo, kuwataarifu viongozi wote wa vyama vya ushirika wilaya hiyo kuwa bei ya pamba imefikia shilingi 900 kwa kilo moja.

Aidha amepiga marufuku machinga wanaowanunua pamba kwa wakulima kwa bei ya chini tofauti na maelekezo ya serikali, na kuongeza kuwa hadi sasa amewakamata viongozi tisa wa vyama vya ushirika ambao walikuwa wakifanya udanganyifu wakati wa ununuzi wa zao la pamba.

John Kabole ambaye ni opereshenu kutoka kampuni ya Alliance ginnery, alisema wao kama kampuni ya ununuzi wa pamba wako tayari kununua pamba kwa bei ya shilingi 900 kwa kilo kutokana na kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa kiwanda na kwamba hitaji lao kubwa ni pamba toka kwa wakulima.

Wakieleza namna ambavyo mnada huo umekuwa na faida kwao baadhi ya wakulima wa zao la pamba katika kata ya Nkololo, wamelisema kuwa umewasaidia sana kuwaepusha na manyanyaso ambayo wamekuwa wakiyapata wakati wa kuuuza pamba.

"Nampongeza mkuu wa wilaya hkwa kusimamia ununuzi wa pamba ikiwemo kuendesha mnada ambao amepandisha bei kutoka shilingi 850  na kuwa shilingi 900 kwa kilo kwa kushindanisha wanunuzi huku wakulima tukishuhudia" Alieleza Nsiya Ludaya mkazi wa kitongoji cha Isanga-Nkololo

"huko nyuma wakulima tulikuwa tukinyanyaswa kwa kununuliwa pamba yetu  kwa bei ya chini," aliongeza Denela Masuke

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com