Dkt. Hussein Ali Mwinyi amechukua fomu ya kugombea Urais Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), ikiwa ni hatua ya kuelekea kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020.
Akizungumza mara baada ya zoezi hilo lililofanyika visiwani humo, Dkt, Mwinyi ameahidi kufanya kampeni za kistaarabu na kisayansi huku akiweka mbele suala la amani.
Amesema endapo atachaguliwa kuongoza Zanzibar, miongoni mwa mambo ambayo serikali yake itajikita kufanya ni pamoja na kuongeza ajira kwa vijana, kuboresha sekta ya uvuvi, kuboresha bandari na usafiri wa majini, kuongeza idadi ya watalii pamoja na kuwaunganisha wa raia wote bila kujali wanapotokea (Pemba au Unguja), dini zao au ukanda (Kaskazini au Kusini).
Ameongeza kuwa, yeye kutumika kwa miaka 20 katika serikali ya Tanzania si kigezo kuwa hatoshi kuiongoza Zanzibar kwani nafasi hiyo imempa uzoefu mkubwa unaomfanya aamini kwamba ataiongoza Zanzibar kwa mafanikio makubwa.
Dkt. Mwinyi alichaguliwa na CCM kugombea nafasi hiyo baada ya kuwashinda wenzake ndani ya chama, lakini amewatoa hofu wanachama na wakereketwa wa chama hicho kwamba kwa sasa hakuna makundi ndani ya chama na kwamba aliyeshinda na walioshindwa wote wanakuwa kitu kimoja kuelekea uchaguzi.
Social Plugin