Zaidi ya watu 100 wametozwa faini na Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga baada ya kubainika kuunganisha mifumo ya maji taka kutoka katika nyumba zao na kuielekeza kwenye mitaro ya barabara kinyume na sheria ya Mazingira
Kauli hiyo imetolewa jana na Afisa Mazingira wa Halmashauri hiyo, Johanes Mwebesa wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake kuhusiana na namana zoezi hilo lilivyofanyika tangu Januari-Julai 2020 katika maeneo mbalimbali Mjini Kahama.
Alisema kuwa Oparesheni ya mtaa kwa mtaa inaendelea kila siku katika kata 12 zilizopo Mjini kuwa kuwashirikisha maafisa afya wa kata hizo ili kuhakikisha utiririshaji wa maji taka katika mitaro ya barabara linatokomezwa haraka.
“Wakati tunafunga mwaka wa fedha Julai 2020 jumla ya wananchi 120 waliokuwa wametozwa faini ya zaidi ya shilingi milioni 20 kutokana na uchafuzi wa mazingira kutokana na kutozingatia sheria ndogo za halmashauri ya Mji ya Usafi wa Mazingira,”alisema Mwebesa.
Alifafanua kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ili kudhibiti utiririshwaji wa Maji taka katika mitaro kwa kuwahamasisha kujenga makaro ya kuhifadhia maji hayo katika nyumba zao ili kutunza mazingira.
Sambamba na hilo Mwebesa alisema kuwa Halmashauri hiyo inazalisha taka ngumu zaidi ya Tani 100 kwa siku ambapo kwa sasa wametoa zabuni kwa kampuni mbalimbali za uzoaji taka katika kata 20 ili kuhakikisha Mji unakuwa katika hali ya Usafi.
“Nitoe rai kwa wananchi wahakikishe wanalipa tozo za usafi,wasafishe mitaro,maeneo yao ya makazi na biashara pamoja na kuwa na vifaa vya kuhifadhia taka ngumu ili kurahisisha zoezi la usafirishaji wa taka hizo unaotekelezwa na wazambuni mbalimbali waliopewa kandarasi,”alisema Mwebesa.
Mwisho.
Social Plugin