Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya elimu na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli ndio siri iliyopelekea shule nane za serikali kuingia kwenye kumi bora katika matokeo ya kidato cha sita 2020.
Ameyasema hayo jana ofisini kwake Jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu ufaulu wa Shule za sekondari zinazomilikiwa na Serikali katika matokeo ya kidato ya sita.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano Serikali imeendelea kufanya vizuri katika Sekta ya Elimu ambapo kwenye matokeo yaliyotangazwa leo tarehe 21/08/2020 ufaulu umeongezeka kwa wanafunzi wa kidato cha sita kutoka asilimia 98 kwa mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 99.51 kwa mwaka.
Amesema kuwa katika matokeo hayo shule za Serikali nane zimeweza kuingia katika shule kumi bora kwa mara ya kwanza zikiwemo shule za kata 3 ambazo ni Kasimiri, Mwandeti na Dareda.
Amezitaja shule za Serikali zilizoshika nafasi kumi bora kuwa ni Mzumbe, Shule ya wasichana Tabora, shule ya wavulana Tabora, Iiliboru na Kibaha
“Zamani ufaulu wa shule za Serikali ulikuwa mdogo kiasi kwamba wazazi walikuwa hawapendi kuwapeleka watoto wao kusoma katika shule hizo wanapochaguliwa kujiunga na shule hizo, lakini sasa shule hizo zimekuwa na ufaulu mkubwa na kuwa tegemeo kwa wazazi kuwapeleka watoto wao” amesema Waziri Jafo
Waziri Jafo anafafanua kuwa uwekezaji uliofanywa na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli umeleta mabadiliko makubwa katika eneo la taaluma nchini
Aidha. Jafo amewashukuru waalimu, maafisa elimu Mikoa na Wilaya kwa usimamizi uliotukuka wa kuhakikisha vijana wa kidato cha sita wanafaulu vizuri na kuliongezea taifa sifa katika suala zima la sekta ya Elimu.
Amewapongeza Wanafunzi wote wa kidato cha Sita kwa kusoma kwa bidi na kupata ufaulu mzuri japokuwa kulikuwa na changamoto ya ugonjwa wa CORONA nchi ya Tanzania bado waliweka juhudu katika masomo na kufaulu mitihani yao vizuri.
Waziri Jafo anaendelea kusema kuwa Serikali imetumia kiasi cha shilingi trilioni 1.09 katika suala zima la utoaji wa elimu bila malipo ambayo imehamasisha sekta ya Elimu nchini,pia kiasi cha shilingi milioni 588 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu jambo hili limesaidia kuongeza idadi ya ufaulu wa wanafunzi.
Sambamba na hilo amesema kuwa Serikali imeweza kuongeza idadi ya waalimu kwa lengo la kuongeza rasilimali ambao watasaidia kupeleka elimu juu zaidi hali ambayo inapelekea kuongeza ufaulu zaidi nchini.
"Matokeo hayo yameonyesha pia wanafunzi waliopata daraja la kwanza hadi la tatu ni asilimia 97.74, haya ni mafanikio makubwa,malengo yetu yalikuwa kuingiza shule sita za serikali kwenye kumi bora lakini tumeingiza shule nane,huu ni ufaulu uliozidi viwango" amesema Waziri Jafo.