Na Mohamed Saif, Geita
KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesitisha mkataba na Mkandarasi Kampuni ya PET Cooperation Ltd na Al Baruwani Investment Ltd kwa kushindwa kukamilisha kwa wakati mradi wa maji wa Nyamtukuza Wilayani Nyang’hwale, Mkoani Geita.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Mradi, Meneja wa Wakala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Geita, Mhandisi Nicas Ligombi ni kwamba utekelezaji wake umefikia asilimia 65 na ulianza kutekelezwa rasmi Januari 2014 na ulipaswa kukamilika ndani ya miezi sita yaani Julai 2014.
Katibu Mkuu, Mhandisi Sanga alifikia uamuzi wa kusitisha mkataba na Mkandarasi baada ya kutembelea mradi huo Agosti 1, 2020 ili kujionea utekelezaji wake ambapo hakuridhishwa na hatua iliyofikiwa licha ya kuwa Mkandarasi alikwishaelekezwa kuhakikisha unakamilika haraka na viongozi mbalimbali waliowahi kuutembelea na kutoa maelekezo.
“Mkataba ulikuwa wa miezi sita lakini sasa imefika miaka sita na kama sasa ujenzi wake umefikia asilimia 65 kwa hesabu ya haraka inamaanisha kwamba tukimuachia Mkandarasi aendelee tunahitaji miaka mingine mitatu yaani mwaka 2023 ndipo ukamilike, hili halikubaliki,” alifafanua Mhandisi Sanga.
Alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa kampeni Mwaka 2015 aliahidi wananchi watapa maji na haitowezekana awamu yake ya kwanza ya uongozi inamalizika hali yakuwa bado maji hayajawafikia wananchi.
“Mwaka 2015, wakati wa kampeni Rais aliahidi kufikisha maji hapa Karumwa Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale, haitokuwa sawa arudi tena kuomba kura hapa halafu ahadi yake aliyoitoa haijakamilishwa, hili sisi kama Wizara hatuwezi kulikubali,” alisema Katibu Mkuu Sanga.
Alisisitiza kuwa mkandarasi hatopewa muda wa nyongeza kukamilisha ujenzi badala yake alielekeza mradi huo ukamilishwe na wataalamu wa ndani kwa mfumo wa force account ambapo alimuelekeza Mkurugenzi wa Ufundi kutoka Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Deusdedit Magoma kuhakikisha anasimamia maelekezo hayo.
Mhandisi Sanga alitoa siku mbili kwa RUWASA Mkoa wa Geita na Mwanza pamoja na Mamlaka za Maji Geita (GEUWASA), Mwanza (MWAUWASA) na Mamlaka ya Maji Kahama Shinyanga (KASHWASA) kufanya maandalizi ya kuanza ukamilishwaji wa mradi.
“Siku mbili zinawatosha kufanya maandalizi na ikifika Jumatano (Agosti 5, 2020) timu ya wataalam iwe imeripoti kwa Mkuu wa Wilaya tayari kwa kuanza kazi na hakikisheni wataalam wanakuwa hapa muda wote na sio kulala Geita na utekelezaji unapaswa kufanyika usiku na mchana hadi mradi utakapoanza kutoa maji,” alielekeza Katibu Mkuu Sanga.
Alisema kwa kuanzia ifikapo tarehe 5 Agosti, 2020 Wizara itapeleka kiasi cha shilingi milioni 100 na kwamba kabla ya mwezi huu kumalizika fedha nyingine itapelekwa.
Aidha, akizungumzia hali ya ujenzi wa miradi ya maji nchini, Katibu Mkuu Sanga alisema kuna zaidi ya miradi 1,425 inayotekelezwa kwenye maeneo mbalimbali kote nchini ambapo kati yake ipo yenye changamoto na huku akiutaja mradi huo wa Nyamtukuza kuwa mmojawapo baada ya mradi wa Same-Mwanga.
Alisema maamuzi yaliyofikiwa kwa miradi yenye changamoto ni wakandarasi wake kusitishiwa mikataba na miradi hiyo kukamilishwa na wakandarasi wenye uwezo pamoja na wataalam wa ndani kwa mfumo wa force account na kwamba tayari mfumo huo umeonyesha mafaniko kwenye baadhi ya miradi ambayo wakandarasi wameondolewa.
“Hatuwezi kuwabembeleza wakandarasi, miradi yote ya Wizara ya Maji ambayo inasuasua tunakwenda kuwapokonya na tutajenga kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani na pia wakandarasi hao hawatapewa tena kandarasi za miradi ya maji, Serikali hii ya Awamu ya Tano inachohitaji ni kuona ni wananchi wanapata maji, na sio maneno,” alisema Katibu Mkuu Sanga.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Wilson Shimo alimpongeza Katibu Mkuu Sanga kwa maelekezo yake kuhusiana na mradi huo. “Tumefurahishwa na maelekezo yako, tupo tayari kuwapokea wataalam wa wizara utakaowaagiza kukamilisha mradi na tupo tayari kuwezesha makazi yao na maandalizi mengine ili kurahisisha utekelezaji kwani hadi hivi sasa tupo nyuma ya wakati,” alisema Shimo.
Naye Mkurugenzi wa Ufundi kutoka Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Deusdedit Magoma alisema wameyapokea maelekezo na ni wajibu wao kuhakikisha utekelezwaji unaanza mara moja.
“Sisi kama RUWASA hatujaridhishwa na hali ya ujenzi; nimepokea maelekezo na tutajitahidi kuhakikisha tunakamilisha hata kabla ya siku hizo 60 tulizoelekezwa,” alisema Mhandisi Magoma.
Mradi wa Maji wa Nyamtukuza unatarajiwa kunufaisha wakazi 38,000 kutoka vijiji Nyamtukuza, Nyarubele, Nyantukara, Kitongo, Ikangala, Kakora, Kayenze, Izunya, Bukwimba na Kharumwa.
Ziara hiyo Mkoani Geita ni ya kwanza kwa Katibu Mkuu huyo tangu ameteuliwa na kuapshiwa rasmi kushika nafasi hiyo.
Social Plugin