Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesikitishwa na kitendo cha kiwanda cha mbolea za maji cha Isacha Feeders Intertrade cha Moshi mkoani Kilimanjaro kuzalisha bidhaa za mbolea ambazo hazisajiliwa na kuthibitishwa ubora wake kwa wakulima.
Akiwa katika ziara ya kukagua viwanda vya mbolea nchini leo Katibu Mkuu huyo alijionea bidhaa za mbolea ya maji iitwayo “Booster II” ikiwa katika ghala la kiwanda cha Isacha Feeder –Njoro Manispaa ya Moshi na kubaini kuwa haijasajiliwa na mamlaka za uthibiti ubora nchini.
“Sijafurahishwa na utendaji kazi wa kiwanda hiki cha mbolea cha Isacha Feeders kuona mbolea inayozalishwa haijasajiliwa na Shirika la Viwango (TBS ) pia haina Barcode hali inayohatarisha mazao ya wakulima na afya za walaji” alisema Kusaya.
Taarifa ya kiwanda hicho cha mbolea ya maji imeonyesha kilianzishwa mwaka 2016 kikizalisha mbolea ya maji ambazo zinauzwa kwenye maduka mbalimbali nchini bila kuwa na usajili wa ubora toka TBS.
Kufuatia hali hiyo, Katibu Mkuu Kusaya ameagiza wamiliki wa kiwanda hicho kwenda ofisini kwake Dodoma ifikapo tarehe 03 Septemba 2020 ili kujieleza kwanini serikali isichukue hatua za kukifunga kiwanda hicho hadi wakamilishe taratibu za usajili ili kulinda wakulima na uharibifu unaoweza kujitokeza endapo mbolea hiyo ikikosa ubora.
“Ninyi mnazalisha mbolea na kuipeleka kwa wakulima wangu sasa ikitokea mazao ya wakulima yameharibika na mbolea hii isiyo na uthibitisho wa ubora nani atalipia gharama hizo?” alihoji Katibu Mkuu Kusaya Kufuatia hali hiyo Kusaya alitoa maagizo matano kwanza, mmiliki wa kiwanda hicho cha Isacha kuwasilisha taarifa inayoonyesha tangu mwaka 2016 wamezalisha kiasi gani cha mbolea na wameuza wapi, pili wawasilishe uthibitisho wa cheti cha kuendesha kiwanda toka BRELA na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Agizo la tatu mmiliki wa kiwanda mbolea cha Isacha aeleze kwanini kiwanda hakina bango la utambulisho na hakijulikani na uongozi wa mkoa
wa Kilimanjaro mahala kilipo na nne kiwanda hicho kiwasilishe taarifa ya ulipaji kodi serikalini tangu kilipoanza kazi mwaka 2016 hadi sasa. “Mkija Dodoma nataka mje na taarifa kamili kuhusu uhalali wa kiwanda hiki kuwa na sifa za kuzalisha mbolea inayokwenda kutumika na wakulima ili kuishawishi serikali kuwa mnastahili kuendelea ka kazi ” alisisitiza Kusaya.
Kusaya alisema akirejea Dodoma atawaalika Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Mapato (TRA) Shirika la Viwango (TBS), BRELA na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) wajadili hatua za kuchukua dhidi ya viwanda ambavyo vinakiuka taratibu za uzalishaji mbolea nchini.
Naye Msimamizi wa kiwanda hicho cha Isacha Feeder -Njoro, Rajab Issa Juma alisema kiwanda hicho kinazalisha lita 17,000 za mbolea ya maji (Booster II: Foliar Fertilizer for Use in all Crops) kwa mwaka ambapo lita moja huuzwa kwa bei ya shilingi 2,000 kwa wakulima. Awali Katibu Mkuu huyo alitembelea kiwanda cha mbolea ABM cha Tanga kuona hali ya uzalishaji na kukuta kiwanda hicho kikizalisha chokaa kilimo chini ya uwezo wake kutokana na changamoto ya mtaji.
Akizungumza na waandishi wa habari kiwandani hapo Mkurugenzi wa kiwanda hicho Aubray Maimu alisema wanazalisha tani 5,000 za chokaa kilimo (limestone) kati ya lengo la tani 10,005 kufikia mwaka 2021. “Mgodi wetu wa Zange Mkulumuzi hapa Kange Tanga una mawe ya chokaa zaidi ya tani milioni 25 inayotesheleza uzalishaji wa mbolea ya chokaa kwa wakulima” alisema Maimu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephano Ngailo amesema mahitaji ya mbolea nchini ni tani 664,000 wakati uzalishaji katika viwanda vyote 12 umefikia tani 38,000 pekee kwa mwaka. Katibu Mkuu Kusaya yuko katika ziara ya kukagua na kujionea hali ilivyo kwenye viwanda vya mbolea nchini ambapo tayari ametembelea kiwanda cha Mbolea za Asili cha Guavay cha Dar es Salaam ambapo anatarajia kutembelea pia mikoa ya Arusha na Manyara Lengo la ziara hii ni kuhamasisha wawekezaji wa ndani ya nchi na nje kuanzisha viwanda vya mbolea ili wakulima wapate kwa gharama nafuu na karibu na mashamba yao badala ya kutegemea mbolea toka nje.
Social Plugin