Mgombea Urais kupitia chama cha SAU Muttamwega Mgaywa (Kulia), alipowasili ofisi za NEC Dodoma peku akiwa na wenzake.
Mgombe Urais kupitia chama cha Sauti ya Umma (SAU), Muttamwega Mgaywa, ametaja sababu iliyopelekea kwenda kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo akiwa peku bila viatu na kusema kuwa kitendo hicho kinaashiria utetezi wao kwa wakulima kwakuwa hakuna anayelima akiwa na viatu.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Agosti 7, 2020, mara baada ya kuwasili ofisi za NEC Jijini Dodoma, wakiwa peku hali iliyozua maswali na sintofahamu kwa watu wengi, huku wao wakitaja vipaumbele vyao kwamba lengo lao ni kumuinua mkulima kwa kuhakikisha anauza mazao yake kwa bei yenye tija.
"Sisi ni watoto wa wakulima na mkulima halimi na viatu na ndiyo mwenye shida, kuna Watanzania wengi mpaka leo hawana viatu, sisi ndiyo watetezi wa wanyonge tunataka vipaumbele vyetu viwe ni amani, upendo na umoja cha pili ni kilimo tunataka tumkomboe mkulima apate bei nzuri ya Pamba kwa 5000, Korosho 5000 na Kahawa ni 5000 kwa kilo" amesema Muttamwega Mgaywa.
Muttamwega Mgaywa pamoja na mgombea mwenza Satia Mussa wamejitokeza leo katika ofisi za Tume ya Uchaguzi jijini Dodoma kuchukua fomu za uteuzi wa urais kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao wa mwezi Oktoba mwaka huu.
Chanzo - EATV