Wagombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanatarajiwa kujulikana kesho.
Wagombea wa nafasi hiyo Bara na Zanzibar watajulikana baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kuanza kujifungia toka jana kupitia na kujadili majina ya wagombea waliotia nia katika nafasi hiyo.
Jana kamati hiyo ilianza vikao vyake vya mchujo ambavyo vinafanyika kwa siku tatu mfululizo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene, Kamati Kuu ilianza kutafiti majina ya wagombea hao jana, na leo watapigiwa kura na baadaye yatawasilisha kwa Baraza Kuu la chama hicho ambalo linaketi leo.
Makene alisema majina yanayotakiwa kupigiwa kura leo ya wagombea urais ni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mgombea mwenza na mgombea wa nafasi hiyo ya urais upande wa Zanzibar.
Makene alisema baada ya Baraza Kuu kupitisha majina ya wagombea hao kwa Jamhuri na Zanzibar, yatakabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa chama hicho leo ambaye naye atayawasilisha katika Mkutano Mkuu utakaofanyikia kesho kwa ajili ya uamuzi wa mwisho.
Makene alisema pamoja na kujadili majina ya wagombea urais, pia Kamati Kuu hiyo ilijadili ilani ya uchaguzi ya chama hicho ambayo nayo itapitishwa kesho.
Jumla ya watiania saba ndiyo waliorejesha fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo ndani ya CHADEMA akiwamo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, mwingine ni aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Wakili Simba Neo, Leonard Manyama, Gasper Mwanalelya, Lazaro Nyalandu na Dk. Maryrose Majinge.